NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema tuzo walizopata katika Tuzo za Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) ni chachu ya kuimarisha uwazi, uwajibikaji na uaminifu wa wananchi kupitia usimamizi bora wa fedha.
Shirika hilo limeeleza kuwa kutambuliwa huko kunathibitisha juhudi zake za kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa katika uandaaji wa taarifa za fedha, hatua inayolenga kuboresha utendaji na utekelezaji wa majukumu yake katika sekta ya mafuta na gesi nchini.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo zilizotolewa Novemba 26, 2026, katika viwanja vya APC, Mbweni, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue, amesema kutambuliwa huko ni faraja kwa bodi kwa kuwa kunathibitisha juhudi za kuhakikisha shirika linaendeshwa kwa kuzingatia misingi bora ya utawala na usimamizi wa fedha.
Amesema TPDC ni Shirika la Taifa la Mafuta (National Oil Company) lenye majukumu makubwa katika sekta ya mafuta na gesi, hivyo ni muhimu kuhakikisha taarifa zake za kifedha zinaandaliwa kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika kimataifa, hususan kutokana na ushirikiano wake na kampuni mbalimbali za kimataifa.
Ameeleza kuwa taarifa za fedha ni sehemu muhimu ya kuonesha taswira ya shirika, kwa kuwa zinaweka wazi namna linavyosimamia rasilimali zake na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia sera na miongozo ya Serikali.
Aidha, amesema tuzo za NBAA zina mchango mkubwa katika kuhamasisha ushindani chanya miongoni mwa taasisi, kwa kutambua zinazofanya vizuri katika uandaaji wa taarifa za fedha na kuzichochea nyingine kuboresha mifumo ya usimamizi na uendeshaji.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa TPDC, Francis LUpokela, amesema tuzo hizo zimeongeza morali kwa wafanyakazi wa shirika hilo kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia misingi bora ya usimamizi wa fedha.
Amesema kutambuliwa kwa TPDC ni ishara kuwa shirika limekuwa likizingatia taratibu na miongozo mbalimbali katika usimamizi wa fedha na utekelezaji wa majukumu yake.
Lupokela amesema mafanikio hayo yanaimarisha pia uaminifu wa wananchi kwa TPDC, kwa kuwa ni shirika la umma linalotekeleza majukumu yake kwa kutumia rasilimali za umma, ikiwemo fedha zinazotokana na kodi na tozo mbalimbali.
EmoticonEmoticon