Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya teknolojia ya Akili Unde (AI) katika utumishi wa umma ili kuongeza ufanisi wa kazi, kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha maamuzi katika taasisi za serikali.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Dk. Mwinyi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, katika ufunguzi wa Mkutano wa 11 wa Mwaka wa Mtandao wa Mameneja wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma Afrika (APS HRMNET), uliofanyika katika Hoteli ya Verde, Mtoni, Zanzibar alisema maendeleo ya teknolojia yanahitaji nchi za Afrika kuimarisha mifumo ya utumishi wa umma ili kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia.
Alisema matumizi ya Akili Unde yanaweza kusaidia kuchambua taarifa kwa haraka, kurahisisha maandalizi ya mipango na kuboresha huduma kwa wananchi, lakini yanapaswa kuzingatia sheria, maadili, uwajibikaji, uwazi na usalama wa taarifa za wananchi.
Aidha, alisisitiza kuwa mageuzi ya utumishi wa umma yanapaswa kuanzia katika uwekezaji kwa watu kwa kuwajengea watumishi uwezo, maarifa na ujuzi unaohitajika sasa na baadaye, ili kuwa na watumishi wenye weledi, maadili na uwajibikaji.
Akizungumzia nafasi ya vijana katika maendeleo ya teknolojia, alisema takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonesha vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 30 ni asilimia 34.5 ya watu nchini, huku takwimu za utumishi wa umma zikionesha kuwa wanachangia takribani asilimia 40 ya nguvu kazi, hivyo wanapaswa kupewa fursa za kujifunza na kushiriki katika maendeleo hayo.
Akitoa rai kwa washiriki wa mkutano huo, Dk. Mwinyi alisema ni muhimu kujadiliana kwa uwazi, kubadilishana uzoefu na kufikia maazimio madhubuti, yanayotekelezeka na yanayopimika ili kuboresha utumishi wa umma katika nchi za Afrika.
Alisema pia kuwa haiwezekani kufikia Dira ya Maendeleo ya Afrika 2063 bila kuwa na rasilimali watu wenye maarifa, ujuzi, weledi, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo.
Alisema Zanzibar inajivunia kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kuwa sehemu ya jukwaa linalowaunganisha wataalamu na viongozi wa rasilimali watu kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa lengo la kujenga utumishi wa umma wenye ufanisi, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Jakaya Kikwete, alisema mabadiliko ya teknolojia duniani yanahitaji wataalamu wa rasilimali watu kutumia mifumo ya kisasa ili kuimarisha utendaji wa taasisi za umma, huku wakizingatia maadili, sheria na taratibu zilizowekwa.
Alisema teknolojia ya Akili Unde inapaswa kutumika kama nyenzo ya kuchochea maendeleo, kuboresha utendaji na kusaidia kufanya maamuzi yenye tija kwa manufaa ya wananchi wanaohudumiwa na serikali.
Aliongeza kuwa mkutano huo utatoa fursa kwa washiriki kujadili namna ya kukabiliana na mabadiliko yanayotokana na matumizi ya Akili Unde kwa kuzingatia mazingira ya nchi za Afrika na kasi ya maendeleo ya teknolojia.
Naye Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Suleiman Masoud Makame, akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutekeleza taratibu na masharti ya APS HRMNET kwa lengo la kuimarisha utumishi wa umma na kuboresha huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Rais wa Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimali Watu katika Sekta ya Umma Afrika (APS HRMNET), Xavier Daud, alisema mkutano huo unalenga kuwaunganisha wataalamu wa rasilimali watu, washauri na washirika wa maendeleo ili kubadilishana maarifa, kujenga mahusiano na kuandaa mikakati ya kuimarisha utendaji wa sekta ya umma barani Afrika.
Alisema mtandao huo umeendelea kukua, ambapo mkutano wa mwaka 2023 uliofanyika Nairobi, Kenya, ulihudhuriwa na washiriki 120, mwaka 2024 uliofanyika Arusha, Tanzania, ulihudhuriwa na zaidi ya 700, huku mkutano wa mwaka 2025 nchini Sierra Leone ukivutia washiriki 650 na mkutano wa mwaka huu Zanzibar ukiwa na zaidi ya washiriki 1,000.
Alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetenga jengo katikati ya Jiji la Dodoma litakalotumika kuwa makao makuu ya kudumu ya mtandao huo pamoja na kituo cha maarifa na mafunzo kwa wataalamu wa rasilimali watu kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Naye mwakilishi wa Jumuiya ya Wasimamizi wa Utawala wa Umma Afrika (APA), Dk. John Nakabago, alisema matumizi ya Akili Unde katika sekta ya umma yanapaswa kuzingatia utu, maadili, uwajibikaji na maslahi ya wananchi, akisisitiza kuwa teknolojia hiyo inapaswa kuwa nyenzo ya kuongeza ufanisi badala ya kuchukua nafasi ya binadamu.
Alisema pamoja na fursa zinazotokana na teknolojia hiyo, ni muhimu kuzingatia ulinzi wa taarifa, upendeleo wa mifumo ya kiteknolojia, uwazi katika maamuzi na upatikanaji sawa wa huduma ili kulinda haki za wananchi na kuimarisha imani yao kwa taasisi za umma.





















EmoticonEmoticon