AFYA YA MAZINGIRA KUWA NGUZO YA MAANDALIZI YA TANZANIA KUIHUDUMIA AFCON 2027

November 19, 2026

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Dkt. Samweli Lazaro,akizungumza wakati akifungua Kongamano la Usafi wa Mazingira lililoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Matumizi ya Choo Bora Duniani kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Grace Magembe.

Na .Mwandishi Wetu- DODOMA

WATAALAMU  wa afya ya mazingira nchini wametakiwa kuimarisha mikakati ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko, hususan Ebola, kwa kuongeza ufuatiliaji wa afya mipakani, huduma za unawaji mikono na utayari wa timu za kukabiliana na dharura, ili kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini na kusambaa kwa jamii.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Dkt. Samweli Lazaro, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Grace Magembe,wakati akifungua Kongamano la Usafi wa Mazingira lililoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Matumizi ya Choo Bora Duniani.

Amesema  kuwa Tanzania ipo katika mazingira yanayohitaji tahadhari kutokana na taarifa za Ebola katika baadhi ya nchi za Afrika na hatari ya maambukizi kuvuka mipaka.

"Wataalamu hao wana nafasi muhimu ya kuzuia maambukizi kwa kusimamia unawaji wa mikono, ukaguzi wa wasafiri katika mipaka rasmi na kuhakikisha timu za kukabiliana na dharura kwenye mikoa na Halmashauri zinakuwa tayari kutoa huduma kwa haraka pale mtu anapohisiwa kuwa na ugonjwa huo."amesema Dkt.Lazaro

Aidha, amesisitiza umuhimu wa mifumo ya ufuatiliaji kubaini watu waliokuwa na mawasiliano na mtu anayehisiwa kuwa na Ebola ili kudhibiti uwezekano wa maambukizi kusambaa katika jamii.

Akizungumzia maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON 2027, Dkt. Lazaro amesema sekta ya afya ina wajibu wa kuhakikisha mazingira ya miji na maeneo mbalimbali yanakuwa safi na salama kwa wageni watakaotembelea nchini.

Aidha, amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) itaendelea kuhakikisha wataalamu wa afya ya mazingira wanapata mazingira wezeshi ya kutekeleza majukumu yao bila vikwazo. Ameeleza kuwa usimamizi madhubuti wa afua za afya ya mazingira una mchango mkubwa katika kuzuia magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira na kupunguza gharama za matibabu.

Dkt. Lazaro amewataka washiriki wa kongamano hilo kutumia siku mbili za majadiliano kuweka maazimio yanayotekelezeka kuhusu changamoto za sasa za afya ya mazingira, hususan maandalizi ya kukabiliana na El Niño, udhibiti wa Ebola na uimarishaji wa huduma za usafi.

Amesema kongamano hilo linapaswa kutoa mikakati itakayowezesha wataalamu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuchangia katika kupunguza mzigo wa magonjwa nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Afya na Mazingira na Usafi  Dkt. Amour Seleman amesema huduma za afya ya mazingira na usafi ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za kiafya zinazolikabili Taifa, ikiwemo magonjwa ya mlipuko, uchafuzi wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema Tanzania inakabiliwa na vitisho vya magonjwa yanayovuka mipaka kama Ebola inayoendelea kuripotiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kipindupindu kinachoripotiwa nchini na katika nchi jirani.

Dkt.Seleman amesema umuhimu wa kuimarisha afua hizo unatokana pia na azma ya Serikali kuhakikisha kaya zote zinakuwa na vyoo ifikapo mwaka 2030, kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Amesema magonjwa mengi yanayoweza kuzuilika bado yanaendelea kuchangia idadi ya wananchi wanaofika kupata huduma za matibabu hospitalini, huku uchafuzi wa mazingira ukichangia pia ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.

Ameeleza kuwa hali hiyo inaweza kuongeza gharama za huduma za afya na kuathiri uendelevu wa Bima ya Afya kwa Wote, hivyo wataalamu wa afya ya mazingira wanapaswa kuimarisha juhudi za kuondoa vihatarishi vya magonjwa katika jamii.

Aidha, amesema kongamano hilo lenye kaulimbiu isemayo Usafi wa Mazingira na Usawa wa Kijinsia limelenga kuweka mikakati endelevu ya kuboresha huduma za afya ya mazingira na kudhibiti magonjwa ya mlipuko, kupitia tathmini ya utekelezaji wa usafi katika makazi, masoko na taasisi, kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya vyoo bora, unawaji mikono, hedhi salama, udhibiti wa taka na upatikanaji wa maji safi na salama.

Amesema mijadala ya siku mbili inatarajiwa kubaini changamoto na kuweka mikakati ya utatuzi, ikiwemo matumizi ya tafiti, ubunifu na ushirikishwaji wa sekta binafsi.

Naye  Mkuu wa Sehemu ya Afya na Usafi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Seleman Yondo, amesema wanatarajia kupata maazimio yatakayoboresha utekelezaji wa afua za afya ya mazingira na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, inayosimamia sera, na TAMISEMI inayofanya utekelezaji lakini pia wadau wengine wanaotekeleza miongozo hiyo.

Aidha, Yondo amependekeza kuundwa kwa Kikundi Kazi cha Kitaalamu cha Afya ya Mazingira ili kusaidia kuboresha miongozo na kuhakikisha inazingatia mahitaji halisi ya utekelezaji. Amesema ushirikiano wa karibu kati ya wizara hizo ni muhimu ili kuimarisha huduma za afya ya mazingira nchini.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Dkt. Samweli Lazaro,akizungumza wakati akifungua Kongamano la Usafi wa Mazingira lililoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Matumizi ya Choo Bora Duniani kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Grace Magembe.

Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Dkt. Samweli Lazaro (hayupo pichani) wakati akifungua Kongamano la Usafi wa Mazingira lililoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Matumizi ya Choo Bora Duniani kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Grace Magembe.

Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Dkt. Samweli Lazaro (hayupo pichani) wakati akifungua Kongamano la Usafi wa Mazingira lililoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Matumizi ya Choo Bora Duniani kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Grace Magembe.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Dkt. Samweli Lazaro akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua  Kongamano la Usafi wa Mazingira lililoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Matumizi ya Choo Bora Duniani kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Grace Magembe.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Dkt. Samweli Lazaro akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua  Kongamano la Usafi wa Mazingira lililoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Matumizi ya Choo Bora Duniani kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Grace Magembe.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »