Na. OWM (KAM),Thailand
Serikali ya Tanzania inalenga kutumia uzoefu wa Thailand kuboresha huduma za fidia na utengamao kwa wafanyakazi wanaopata madhara yatokanayo na kazi, ili kuwawezesha kurejea kazini na katika shughuli za kiuchumi.
Hayo yamebainishwa (Oktoba 21,2026) wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu, nchini Thailand, yenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika sekta ya hifadhi ya jamii na kujifunza mifumo bora ya utoaji wa huduma za fidia na utengamao.
Katika ziara hiyo, Mhe. Sangu alikutana na Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Hifadhi ya Jamii ya Thailand, Bi. Kanchana Poolkaew, na kubadilishana uzoefu kuhusu mifumo ya hifadhi ya jamii na namna bora ya kuwahudumia wafanyakazi waathirika wa kazi.
Aidha, alitembelea Kituo cha Utengamao kilichopo Mkoa wa Kati wa Thailand, kinachotoa huduma za matibabu, ushauri wa kisaikolojia na mafunzo ya ujuzi mbadala kwa wafanyakazi waliopata majeraha au ulemavu unaotokana na kazi.
Ujumbe wa Tanzania ulipata fursa ya kujifunza namna Thailand inavyounganisha matibabu na utengamao na mikakati ya kuwawezesha wafanyakazi kurejea katika ajira zao za awali au kupata ajira mbadala zinazozingatia uwezo wao baada ya madhara.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, zaidi ya asilimia 54 ya wafanyakazi wanaopata huduma kupitia mfumo huo hupona kabisa na kurejea kwa waajiri wao, huku wengine wakisaidiwa kupata fursa mbadala za ajira.
Akizungumzia umuhimu wa ushirikiano huo, Mhe. Sangu alisisitiza ujenzi wa mfumo wa fidia unaomwangalia mfanyakazi kwa mapana, kwa kuzingatia si tu stahiki za kifedha, bali pia urejeshaji wa afya, uwezo wa kufanya kazi na ustawi wa kisaikolojia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, alisema WCF ipo katika hatua za kuanzisha kituo cha utengamao kwa kushirikiana na wadau wenye uzoefu, wakiwemo kutoka Thailand.
Ameeleza kuwa kituo hicho kitakuwa hatua muhimu katika kuimarisha huduma za utengamao, kwa kuwawezesha wafanyakazi walioathirika kupata matibabu na huduma za kurejesha uwezo wa kufanya kazi na kurejea katika ajira.
Ziara hiyo inafanyika katika muktadha wa Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya Tanzania na Thailand, unaoweka msingi wa kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo endelevu ya kuwalinda wafanyakazi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Mwisho.





EmoticonEmoticon