NSSF YASISITIZA HUDUMA BORA KWA VITENDO

October 06, 2026

Na Oscar Assenga, TANGA

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umesisitiza umuhimu wa utoaji wa huduma bora kwa wateja kwa vitendo, ukieleza kuwa huduma hiyo ni msingi muhimu katika kuwafanya wanachama kuendelea kuwa na imani na mfuko huo.

Hayo yameelezwa na Kaimu  Meneja wa NSSF Mkoa wa Tanga Amina Mbuguni wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, ambayo huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango wa wateja katika kuendelea kwa taasisi kutoa huduma zake.

Alisema wiki hiyo ni fursa muhimu kwa NSSF kutafakari namna inavyowahudumia wateja, kusikiliza mahitaji yao na kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa.

“Kaulimbiu ya mwaka huu ya Huduma Bora kwa Vitendo inatukumbusha kwamba ubora wa huduma hauishii kwenye maneno, bali unapaswa kuonekana kwa vitendo katika kila hatua ambayo tunamhudumia mteja,” alisema.

Kwa mujibu wa Kaimu meneja huyo, NSSF imeendelea kupiga hatua katika maeneo mbalimbali ikiwamo uandikishaji wa wanachama, ukusanyaji wa michango, uwekezaji na ulipaji wa mafao.

Alisema hadi Juni 30, 2026, thamani ya Mfuko imefikia Sh trilioni 11.4, ikilinganishwa na Sh trilioni 9.84 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2025.

Aidha, alisema idadi ya wanachama imeongezeka kutoka milioni 1.6 hadi milioni 2.1 kufikia Juni 30, 2026, sawa na ongezeko la asilimia 33.

Alifafanua kuwa kati ya wanachama milioni 2.1, wanachama milioni 1.5 wanatoka katika sekta rasmi, huku 592,791 wakiwa waliojiajiri waliojiunga kupitia Skimu ya Hifadhi.

“Maendeleo haya yanaonyesha juhudi za kuimarisha Mfuko na kupanua wigo wa hifadhi ya jamii, ikiwamo kuwafikia wananchi waliojiajiri kupitia skimu mbalimbali,” alisema.

Katika eneo la utoaji huduma, alisema NSSF imeendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuwawezesha wateja kupata huduma kwa urahisi zaidi.

Alisema kupitia NSSF Portal, waajiri, wanachama na wastaafu wanaweza kupata huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao, zikiwamo kufuatilia taarifa za michango, kujisajili, kufungua na kufuatilia madai ya mafao pamoja na kufanya uhakiki wa wastaafu kidijitali bila kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.

Alisema maboresho hayo yameendelea kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na ulipaji wa mafao, ambapo wastani wa muda wa kulipa mafao umepungua kutoka siku 63 katika mwaka wa fedha 2021/22 hadi siku 19 katika mwaka wa fedha 2025/26.


Kutokana na maboresho hayo, meneja huyo amewasihi wanachama kutumia huduma za kidijitali za Mfuko, hususan katika kufungua na kufuatilia madai ya mafao kwa njia ya mtandao.


Alisema matumizi ya huduma hizo yatawasaidia wanachama kurahisisha upatikanaji wa huduma, kuokoa muda na kupunguza ulazima wa kufika katika ofisi za Mfuko.


Aidha, alisema NSSF inaendelea kuwafikia wananchi waliojiajiri na wanaofanya shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa ajili ya kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii na kuwahamasisha kujiunga na Mfuko.





Share this

Related Posts

Previous
Next Post »