WANANCHI NGORONGORO WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO KWA WATAALAMU WA TATHMINI YA KITUO CHA FORODHA

October 09, 2026

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Luteni Kanali Robert Augustino Kakomangile, kuangalia eneo linalopendekezwa kuwekwa Kituo cha kutoa huduma za Forodha, katika Kijiji cha Njoroi, Kata ya Ololosokwan, Tarafa ya Loliondo Mkoa wa Arusha katika mpaka wa Tanzania na Kenya.


***************

Na. Peter Haule, WF, Ngorongoro.

Wananchi wa Ngorongoro mkoa wa Arusha wametakiwa kutoa ushirikiano kwa wataalamu wanaofanya tathmini ya uhitaji wa kuanzishwa kwa Kituo cha Huduma za Forodha katika eneo hilo, ili kubaini iwapo eneo hilo linakidhi vigezo vya kisheria na kiutendaji vya kuwa na kituo hicho.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Njoroi, Kata ya Ololosokwan, Tarafa ya Loliondo katika mpaka wa Tanzania na Kenya, eneo linalopendekezwa kuwa na Kituo cha Forodha.

Mhe. Munde alisema ni muhimu wananchi kutoa ushirikiano na taarifa sahihi kwa wataalamu wanaotathmini eneo hilo, akisisitiza kuwa taratibu zote za kisheria zinapaswa kufuatwa kabla ya Serikali kufanya uamuzi kuhusu uanzishwaji wa kituo hicho.

Amesema iwapo eneo hilo litakidhi vigezo, Serikali itahakikisha hatua hiyo inaleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Amesema taarifa zitakazokusanywa na timu ya wataalamu zitatolewa kwa wananchi, akieleza kuwa Serikali inasisitiza misingi ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha, Mhe. Munde amesema Serikali ni sikivu kwa wananchi wake na kwamba ziara yake katika eneo hilo imefanyika kufuatia hitaji lililowasilishwa bungeni na Mwakilishi wa wananchi, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, Mhe. Yannick Ndoinyo.

Amesema Serikali ina mpango mzuri katika kutekeleza Dira ya Taifa 2050, ambayo inalenga kuchochea maendeleo ya uchumi na kuongeza fursa za wananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji.

Kutokana na hilo, amewataka wananchi wa Ngorongoro kushiriki kikamilifu katika jitihada za Serikali za kuleta maendeleo na kuchangia katika kufikia malengo yaliyowekwa kupitia Dira hiyo.

Mhe. Munde pia amewashukuru wananchi kwa mapokezi makubwa waliyompa wakati wa ziara hiyo, akiahidi kufikisha salamu zao za pongezi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa jitihada za Serikali katika kuwapelekea wananchi wa eneo hilo maendeleo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ngorongoro, Mhe. Yannick Ndoinyo, amemshukuru Naibu Waziri Munde kwa kutimiza ahadi yake ya kufika katika eneo hilo na kujionea mwenyewe shughuli za kiuchumi zinazofanywa na wananchi.

Mhe. Ndoinyo amesema ujio wa Naibu Waziri umeongeza morali kwa wananchi katika kuendelea na shughuli zao za kiuchumi, huku akieleza kuwa ziara hiyo imekuwa muhimu katika kuwasilisha mahitaji ya wananchi na kuyaona yakifanyiwa kazi kupitia taratibu za Serikali.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Njoroi, Kata ya Ololosokwan, Tarafa ya Loliondo eneo linalopendekezwa kuwekwa Kituo cha Huduma za Forodha, wakati wa ziara yake ya kujionea uhitaji wa Kituo cha kutoa huduma za Forodha katika eneo hilo lililopo mpaka wa Tanzania na Kenya.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Luteni Kanali Robert Augustino Kakomangile, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Njoroi, Kata ya Ololosokwan, Tarafa ya Loliondo, eneo linalopendekezwa kuwekwa Kituo cha Huduma za Forodha, kuhusu umuhimu wa kulinda usalama wakati wa ziara Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), katika eneo hilo.

Kamishna wa Uhamiaji Divisheni ya Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka, Fakih Nyakunga, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Njoroi, Kata ya Ololosokwan, Tarafa ya Loliondo Arusha, eneo lililopo mpakani mwa Tanzania na Kenya, kuhusu kuzingatia taratibu za uhamiaji, wakati wa  ziara ya Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) eneo hilo.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), pamoja na  viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro na Uhamiaji, wakiwa wamevaa vazi la kimasai walilopewa zawadi na wananchi wa  kijiji cha  Njoroi, Kata ya Ololosokwan, Tarafa ya Loliondo Arusha, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) kujionea uhitaji wa Kituo cha kutoa huduma za Forodha eneo hilo.

Mbunge wa Ngorongoro, Mhe. Yannick Ndoinyo, akieleza umuhimu wa kukuza shughuli za kiuchumi katika mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo kijiji cha  Njoroi, Kata ya Ololosokwan, Tarafa ya Loliondo Arusha, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) kujionea uhitaji wa Kituo cha kutoa huduma za Forodha.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Uhamiaji na wananchi wa kijiji cha  Njoroi, Kata ya Ololosokwan, Tarafa ya Loliondo Arusha, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) kujionea uhitaji wa Kituo cha kutoa huduma za Forodha eneo hilo.

Wananchi wa kijiji cha Njoroi, Kata ya Ololosokwan, Tarafa ya Loliondo Arusha, wakiwa tayari kumpokea Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) aliefika eneo hilo lililopo mpaka wa Tanzania na Kenya kujionea uhitaji wa Kituo cha kutoa huduma za Forodha.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »