NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeungana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kufanya usafi katika maeneo ya Posta, sambamba na kukabidhi vifaa vya usafi kwa halmashauri hiyo ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha usafi wa mazingira na kuzuia majanga yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa leo, Oktoba 10, 2026, kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, aliyeambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya zoezi la usafi lililoshirikisha watumishi wa TTCL.
Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Mpogolo ameishukuru TTCL kwa kuona umuhimu wa kushiriki katika kutekeleza maelekezo ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufanya usafi katika jiji la Dar es Salaam.
Amesema usafi wa mazingira ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya taifa na kulinda afya za wananchi, huku akieleza kuwa vifaa vilivyotolewa vitasaidia kurahisisha shughuli za usafi, ikiwemo kuondoa taka na kuzibua mitaro ili kuruhusu maji kupita vizuri wakati wa mvua.
Aidha, amezitaka taasisi na mashirika mengine kuunga mkono juhudi hizo kwa kushiriki kikamilifu katika usafi wa mazingira, akisisitiza kuwa kila taasisi ina wajibu wa kuhakikisha maeneo yanayoizunguka yanakuwa safi.
Mpogolo amewashukuru pia wenyeviti wa serikali za mitaa, madiwani na maofisa afya kwa kushiriki katika zoezi la usafi lililofanyika katika mitaa yote 159 ya Wilaya ya Ilala.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa TTCL, Mhandisi Cecil Francis, aliyekabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, amesema TTCL imeamua kuunga mkono maelekezo ya Rais na viongozi wengine wanaohamasisha usafi wa mazingira kama utamaduni wa kila siku na njia ya kuzuia majanga yanayoweza kutokea wakati wa mvua kubwa.
Amesema kutosafishwa kwa mitaro kunaweza kusababisha maji kushindwa kupita vizuri na kuongeza hatari ya kutokea kwa majanga, hivyo amepongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuchukua hatua za kuhamasisha usafi.
Mhandisi Francis ameongeza kuwa TTCL itaendelea kushiriki katika juhudi za kuboresha mazingira huku ikiendelea kutekeleza jukumu lake la kutoa huduma bora za mawasiliano kwa wananchi.

























EmoticonEmoticon