-Ufadhili wa moja kwa moja wafikia wanufaika 313,882, huku SCGS ikiwezesha zaidi yaShilingi bilioni 192 kwa kupitia taasisi washirika za kifedha
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeeleza kuwa imeendelea kuchochea maendeleo ya mnyororo wa thamani wa kahawa nchini kupitia ufadhili wa moja kwa moja wa Shilingi bilioni 475.83 kwa miradi 38, huku pia ikipanua upatikanaji wa fedha kwa wakulima na wadau wa minyororo ya thamani ya kilimo kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (Smallholder Credit Guarantee Scheme – SCGS), ambao umewezesha zaidi ya Shilingi bilino 192 kutolewa kupitia taasisi washirika za kifedha.
Ufadhili wa moja kwa moja wa TADB katika mnyororo wa thamani wa kahawa umefikia wanufaika 313,882, wakiwemo wanawake 61,202, wanaume 252,680 na vijana 54,794.
Ufadhili huo unaelekezwa katika shughuli mbalimbali za mnyororo wa thamani, kuanzia uzalishaji wa kahawa, ukusanyaji na usimamizi baada ya mavuno, uhifadhi, uchakataji, uongezaji thamani hadi kuwezesha upatikanaji wa masoko.
Akizungumza kwenye Kahawa Festival 2026 inayofanyika Moshi – Mkaoni Kilimanjaro kuanzia tarehe 8 hadi 10 Oktoba 2026, Meneja wa TADB Kanda ya Kaskazini, Bw. Alphonce Mokoki, amesema kahawa ni zao linaloongoza kwa kiwango cha ufadhili katika kitabu cha benki, kutokana na umuhimu wake katika kukuza Uchumi wa mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Kwa TADB, mafanikio ya ufadhili wa kilimo hayapimwi kwa kiasi cha fedha kilichotolewa pekee, bali kwa athari zinazotokana na fedha hizo. Tunataka kuona wakulima wakiongeza tija, vyama vya ushirika vikiwa na uwezo mkubwa zaidi, shughuli za uchakataji na biashara ya kahawa zikikua, thamani ya zao ikiongezeka na fursa za masoko zikiimarika. Tunatarajia kuona uwekezaji huu ukibadilisha maisha na kuongeza ustawi wa wananchi,” alisema Bw. Mokoki.
Alisema TADB haitumii njia moja pekee katika kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa sekta ya kilimo, bali inatumia pia ubia na taasisi nyingine za kifedha kupitia SCGS ili kupanua wigo wa wakulima na wadau wengine kupata mikopo.
“Kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo, TADB inafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi washirika za kifedha, zikiwemo benki na taasisi nyingine za kifedha, ili kuwezesha mikopo kwa wadau wa minyororo ya thamani ya kilimo. Mpaka sasa, kupitia utaratibu huu, Shilingi bilioni 192.21 zimewezeshwa kutolewa kwa walengwa kupitia taasisi washirika 20 za kifedha. Hii inatuwezesha kufikisha fedha za kilimo kwa wigo mpana zaidi wa wakulima na wafanyabiashara wa kilimo,” alisema.
Amesema TADB inawezesha mnyororo mzima wa thamani, kwa kuunga mkono shughuli mbalimbali kuanzia uzalishaji wa kahawa shambani, ukusanyaji, usimamizi baada ya mavuno, uhifadhi, uchakataji, uongezaji thamani hadi upatikanaji wa masoko.
“Kahawa haianzi na kuishia shambani. Kuna safari kutoka kwa mkulima hadi kwenye ukusanyaji, uhifadhi, uchakataji, uongezaji thamani na utafutaji wa masoko. Kila hatua ina umuhimu katika kuhakikisha thamani inayotokana na kahawa inaongezeka na manufaa yake yanawafikia wadau mbalimbali, hususan wakulima. Jukumu la TADB ni kuchochea upatikanaji wa fedha na uwekezaji katika hatua mbalimbali za mnyororo huu,” alisema.
Miongoni mwa wadau wa mnyororo wa thamani wa kahawa walionufaika na ufadhili wa TADB ni Chama cha Ushirika cha Kagera (KCU), Chama cha Ushirika Wilaya ya Karagwe (KDCU), Ngara Farmers, WAMACU ya Mara, Wahurumie AMCOS ya Horongo Mbalizi, Kiwanda cha GDM huko Mbozi na Mbozi Coffee Curing Company Limited, hawa miongoni mwa wengine wengi.
Kupitia ufadhili huo, TADB pia inawezesha uwekezaji katika miundombinu ya uhifadhi na maghala, pamoja na miundombinu ya uchakataji na shughuli nyingine muhimu za baada ya mavuno.
Hatua hii inalenga kupunguza upotevu na changamoto za baada ya mavuno, kuongeza ubora wa kahawa na kuwezesha wadau kuwa na uwezo bora wa kuhifadhi na kuuza mazao kwa wakati unaofaa.
Aidha, TADB inaendelea kusisitiza umuhimu wa kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi katika mnyororo wa thamani wa kahawa, kwa kuhimiza uwekezaji na uzalishaji unaolenga kuongeza ustahimilivu wa wakulima na biashara za kilimo dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), vyama vya ushirika, vyama vya wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta ya kahawa, TADB inaendelea kuchochea upatikanaji wa mitaji na uwekezaji unaolenga kuimarisha mnyororo wa thamani na kuongeza ushindani wa kahawa ya Tanzania.
“Tunataka kuona kahawa ya Tanzania ikiendelea kuwa na thamani zaidi, wakulima wakipata tija na kipato zaidi, biashara za kilimo zikikua na uwekezaji katika uchakataji na uongezaji thamani ukiongezeka. Hii ndiyo maana ya TADB kuwepo si kutoa fedha pekee, bali kutumia fedha kama kichocheo cha mabadiliko katika kilimo na maisha ya wananchi,” alisisitiza Bw. Mokoki.
TADB inatumia ushiriki wake katika Kahawa Festival 2026 kuendelea kutoa elimu na kuongeza uelewa miongoni mwa wakulima, wadau wa mnyororo wa thamani, vyombo vya habari na umma kuhusu fursa za ufadhili na namna Benki inavyoshirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza sekta ya kahawa nchini.




EmoticonEmoticon