
Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Juma Homera amesema mkakati wa pamoja wa kuelimisha matumizi ya nishati safi ya kupikia utachangia idadi kubwa ya wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo sio salama hivyo kufanikisha kwa vitendo malengo ya Serikali ya kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2034 asilimia 80 ya watanzania wanatumia nishati safi
Mhe. Homera ameyasema hayo leo, Oktoba 24, 2026, wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma, wakati akiongoza mbio za Site Trust Nishati Safi Marathon 2026, zilizolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza katika Banda la TANESCO Waziri Homera amesema kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 ni jukumu linalohitaji mikakati madhubuti na ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kuhamasisha wananchi kuachana na nishati zisizo salama na kuhamia kwenye nishati safi.
Ameipongeza TANESCO kwa kuanzisha mpango wa kuwawezesha wananchi kupata majiko yanayotumia umeme kwa kulipa kidogo kidogo kupitia manunuzi ya umeme wa LUKU.
Amesisitiza kuwa mpango huo unapaswa kutangazwa zaidi na kuwafikia wananchi wengi , hususan wanaoishi maeneo ya vijijini.
“TANESCO mnafanya kazi nzuri sana, si tu katika kutekeleza miradi ya umeme, bali pia kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme. Natoa rai kwenu, mpango huu wa ukopeshaji majiko kwa wananchi utangazwe kwa upana zaidi kwa kuwa unagusa moja kwa moja maisha ya wananchi wa mijini na vijijini,” alisisitiza Mhe. Homera.
Kwa upande wake, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Wadau wa TANESCO, Bw. Augustino Kasale, amesema Shirika linaendelea kutumia majukwaa mbalimbali kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme, ikiwemo matumizi ya majiko yanayotumia umeme kwa ufanisi, kwa lengo la kupunguza gharama za kupikia, kulinda afya za wananchi na kutunza mazingira.
“TANESCO inaendelea kutekeleza mpango wa ukopeshaji majiko kwa wananchi kwa kutambua umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Aidha, tunaendelea kutumia majukwaa mbalimbali kutoa elimu hiyo kama sehemu ya jitihada za kuunga mkono ajenda ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi. Mwitikio wa wananchi wanaohitaji na kutumia majiko haya ni mkubwa,” alifafanua Bw. Kasale.
Katika hatua nyingine, Waziri Homera alikabidhi gari kwa TANESCO wilayani Namtumbo kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za umeme kwa wananchi wa Tarafa ya Lusewa, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
Aidha, washindi wa mbio za Site Trust Nishati Safi Marathon 2026 walikabidhiwa majiko yanayotumia umeme kwa ufanisi ili kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kuhusu faida za kutumia umeme kupikia.








EmoticonEmoticon