
Na Mwandishi Wetu, KOROGWE
KOROGWE. Soka limeendelea kuwa zaidi ya mchezo wa dakika 90, likigeuka kuwa jukwaa la kuibua vipaji, kufungua milango ya ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa jamii, safari ambayo mashindano ya Hale Cup yameendelea kuisimamia kwa vitendo.
Hilo limebainika baada ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Zaituni Swai, kufungua rasmi mashindano ya Hale Cup msimu wa 2026/2027, yanayoshirikisha timu 32 kwa lengo la kukuza vipaji vya vijana na kuibua wachezaji watakaoweza kufikia viwango vya juu vya soka.
Akizungumza katika ufunguzi wa mashindano hayo, Swai amewapongeza waandaaji wakiongozwa na Mkurugenzi Dkt. Hassan Abasi kwa kuendelea kuwekeza katika michezo na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwawezesha vijana kutumia vipaji vyao kama nyenzo ya kujiletea maendeleo.

Amesema michezo ina nafasi kubwa katika jamii kwa kuwa, mbali na kutoa burudani, ni njia ya kujenga afya, kudumisha amani, kuimarisha umoja na kufungua fursa za kiuchumi kwa vijana.
“Tunatambua michezo si burudani pekee, bali ni ajira, afya na amani. Inawaunganisha vijana na kuwapatia fursa mbalimbali za kuendeleza vipaji vyao na kujikwamua kiuchumi,” amesisitiza Swai.

Ameongeza kuwa juhudi hizo zinaendana na dhamira ya kukuza maendeleo ya vijana kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Wakati macho ya mashabiki yakielekezwa kwa wachezaji wanaowania ushindi uwanjani, wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali nao wameonekana kuwa miongoni mwa wanufaika wa mashindano hayo.

Swai amesema mikusanyiko ya mashabiki wakati wa mechi inatoa nafasi kwa wajasiriamali kuuza bidhaa na huduma mbalimbali, jambo linalochangia kuongeza mzunguko wa fedha na kuchochea uchumi wa wakazi wa Korogwe.
Amesema uwepo wa wafanyabiashara, wakiwemo wanawake wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kujipatia kipato, unaonyesha namna michezo inavyoweza kuunganisha burudani na maendeleo ya wananchi.

Kwa msingi huo, amewataka waandaaji kuendelea kupanua wigo wa mashindano hayo kwa kuwashirikisha wadau wengi zaidi.
Hata hivyo, Swai ametoa ombi maalumu kwa waandaaji kuhakikisha kuwa misimu ijayo inajumuisha timu za wanawake ili kuongeza ushiriki wao, kukuza vipaji vyao na kuifanya michuano hiyo kuwa jukwaa jumuishi zaidi.

Akizungumzia maandalizi na malengo ya msimu huu, Mratibu wa Hale Cup 2026/2027, Madau Manywele, amesema jumla ya timu 32 zinashiriki mashindano hayo yanayolenga kutoa nafasi kwa vijana kutoka maeneo mbalimbali kuonyesha uwezo wao.
Manywele amesema uamuzi wa kushirikisha timu kutoka nje ya Korogwe na mkoa wa Tanga unalenga kuongeza ushindani, kupanua wigo wa vipaji na kuwapa wachezaji nafasi ya kupima uwezo wao dhidi ya wapinzani kutoka mazingira tofauti ya soka.

Miongoni mwa timu zinazoshiriki ni Avocado ya Dar es Salaam, Fountain Gate ya Morogoro na Mwana United ya Moshi.
Pia, mashindano hayo yamevutia timu zenye historia katika soka la mkoa wa Tanga, zikiwemo African Sports, Jogoo FC na Mkurumuzi kutoka Tanga Mjini.

Kwa mujibu wa Manywele, mchanganyiko huo wa timu unalenga kuongeza ushindani na kuwapa vijana jukwaa la kuonyesha vipaji vinavyoweza kuwafungulia milango ya kucheza katika klabu kubwa na mashindano ya ngazi za juu.
Hale Cup si jina jipya katika harakati za kukuza soka la vijana. Mashindano hayo yalianza mwaka 2017 na, kwa mujibu wa Manywele, yaliendeshwa kwa takribani miaka mitatu mfululizo chini ya udhamini wa Dkt. Hassan Abasi kupitia Dkt. Abasi Foundation.
Katika kipindi hicho, mashindano yamekuwa yakitoa nafasi kwa vijana kuonyesha vipaji vyao na kupata fursa za kuendelea na soka katika ngazi za juu.
Manywele amesema baadhi ya wachezaji walioibuliwa kupitia mashindano hayo wamepata nafasi ya kucheza Coastal Union ya Tanga, huku wengine wakipata fursa ya kucheza ligi kuu nchini Kenya.

Ameeleza pia kuwa baadhi ya vijana wanaendelea kufanya mazoezi na Azam FC, hatua inayoweza kuwaandalia mazingira ya kusonga mbele katika safari zao za soka.
Mafanikio hayo yanaonyesha umuhimu wa mashindano ya ngazi ya jamii katika kuwatambua wachezaji wenye uwezo na kuwaunganisha na fursa zinazoweza kubadili maisha yao kupitia soka.

Mbali na kutengeneza mazingira ya ushindani wa soka, mashindano hayo yameendelea kuwa jukwaa la shughuli za biashara kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya michezo.
Manywele amesema kipindi cha mashindano huwa na fursa nyingi kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati kutokana na ongezeko la mashabiki na watu wanaofika kushuhudia mechi.

Hali hiyo huwapa wajasiriamali nafasi ya kuongeza mauzo ya bidhaa zao na kupata kipato kinachoweza kuwasaidia kuendesha shughuli zao za kila siku.
Kwa mtazamo huo, Hale Cup imeendelea kuunganisha sekta mbili muhimu katika jamii: michezo kama njia ya kukuza vipaji na biashara kama nyenzo ya kuimarisha maisha ya wananchi.

Hale Cup inaendeshwa chini ya mwavuli wa Hale Festival, jukwaa ambalo pia limekuwa likitoa nafasi kwa vijana wenye vipaji vya muziki na burudani kuonyesha uwezo wao.
Ushirikiano huo unaongeza wigo wa fursa kwa vijana, kwa kuwakutanisha wale wanaopenda michezo na wale wenye vipaji vya sanaa na burudani.

Mashindano ya Hale Cup msimu wa 2026/2027 yamepangwa kuanza Oktoba 10, 2026 na kuhitimishwa Januari Mosi, 2027.
Kwa kipindi hicho, macho ya mashabiki yatakuwa kwa timu 32 zinazowania ushindi, huku matarajio yakiwa ni kuona vipaji vipya vikiibuliwa na shughuli za kiuchumi zikichochewa katika jamii zitakazonufaika na mashindano hayo.


EmoticonEmoticon