TFC YAHAMASISHA MATUMIZI YA MBOLEA KWA TIJA YA KILIMO

August 01, 2026

Mkurugenzi wa Uendeshaji Biashara wa Kampuni ya Mbolea Tanzania, Lameck Borega,akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea kitaifa katika viwanja vya Dkt.John Samuel Malecela jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) imewahimiza wakulima nchini kuachana na dhana potofu kuhusu matumizi ya mbolea, ikisisitiza kuwa kilimo cha kisasa kinahitaji matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza uzalishaji na tija mashambani.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uendeshaji Biashara wa Kampuni ya Mbolea Tanzania, Lameck Borega, wakati wa Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea kitaifa katika viwanja vya Dkt.John Samuel Malecela jijini Dodoma.

Bw.Borega amesema TFC, ambayo inamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imefika katika maonesho hayo ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kutumia mbolea bora na zinazokidhi mahitaji ya mazao pamoja na aina mbalimbali za udongo.

Amesema kampuni hiyo inasambaza mbolea za aina mbalimbali ikiwemo DAP kwa ajili ya kupandia, Urea na CAN kwa ukuaji wa mazao, pamoja na NPK na SA zinazosaidia kukomaza mazao, huku akisisitiza kuwa uchaguzi wa mbolea unapaswa kuzingatia mahitaji halisi ya udongo na zao husika.

"Kilimo bila mbolea ni kilimo kisicho na tija. Ili mkulima apate mavuno mengi na yenye ubora ni lazima atumie mbolea sahihi," amesema Borega.

Amefafanua kuwa maafisa wa TFC wanaendelea kuwafikia wakulima katika mikoa yote nchini kwa kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, sambamba na kuwasaidia kuelewa aina za mbolea zinazofaa kwa maeneo yao.

Aidha, amesema maonesho ya Nane Nane yamekuwa jukwaa muhimu la kuonesha tofauti ya uzalishaji kati ya mashamba yanayotumia mbolea na yale yasiyotumia kupitia mashamba darasa (demo plots) yaliyoandaliwa na kampuni hiyo.

"Anayetembelea banda letu anaweza kujionea mwenyewe tofauti ya ukuaji wa mazao yaliyotumia mbolea na yale ambayo hayajatumia. Huo ni ushahidi wa moja kwa moja wa faida za matumizi ya mbolea," amesema

Borega pia amewataka wakulima kupuuza imani kwamba mbolea huharibu udongo, akieleza kuwa udongo hutofautiana kwa kiwango cha virutubisho na kwamba mbolea huongeza virutubisho vinavyokuwa vimepungua kutokana na matumizi ya muda mrefu na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amekumbusha kuwa Kampuni ya Mbolea Tanzania ilianzishwa mwaka 1968, miaka minane baada ya Uhuru, ikiwa na dhamira ya kuhakikisha wakulima wanapata mbolea bora kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

"Tunawaalika wakulima wote kutembelea banda letu katika maonesho ya Nane Nane na kufika katika vituo vyetu vilivyopo nchini kote ili kupata mbolea bora zilizothibitishwa na mamlaka husika kwa ajili ya kilimo chenye tija," amesema  Borega.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »