SHERIA YA NHIF KUPANUA WIGO WA WANACHAMA NA KUBORESHA HUDUMA

August 30, 2026

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) uko kwenye mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Sura ya 395, kwa lengo la kupanua wigo wa wanachama, kuendana na mahitaji ya sasa ya huduma za afya na kuimarisha uendelevu wa Mfuko.

Marekebisho hayo pia yanalenga kuimarisha udhibiti wa matumizi mabaya ya Mfuko, ikiwemo udanganyifu unaoweza kufanywa na baadhi ya wanachama, waajiri na watoa huduma za afya lakini kwenda sambamba na sheria Mama ya Bima ya Afya kwa Wote.

Akizungumza  katika ukumbi wa mikutano wa NHIF, Kinondoni, Dar es Salaam, wakati wa kupokea maoni ya wadau kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo, Meneja wa Huduma za Sheria wa NHIF, Matamus Fungo, amesema sheria hiyo iliyotungwa mwaka 1999 inahitaji maboresho ili iendane na mabadiliko yaliyopo katika sekta ya afya na mwelekeo wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

“Tunataka sheria yetu iweze kuboreshwa ili iwezeshe watu wengi zaidi kujiunga na pia kuziba mianya ya matumizi mabaya ya kadi yanayofanywa na baadhi ya wanachama wasio waaminifu” amesema.

Amesema marekebisho hayo yanatarajiwa kuongeza idadi ya wanachama, kuimarisha uendelevu wa Mfuko na kuweka mifumo madhubuti zaidi ya kudhibiti udanganyifu na matumizi yasiyofaa ya huduma za bima ya afya.

Kuzingatia Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Mwenda Tulalemwa, amesema marekebisho ya sheria yanapaswa kuzingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya wananchi pamoja na kuendana na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, ili kuhakikisha hakuna mgongano wa kisheria.

Amesema wadau waliotoa maoni wamependekeza maboresho katika maeneo mbalimbali, ikiwemo mfumo wa malipo kwa vituo vya kutolea huduma za afya, huduma kwa watu wasio na uwezo na watu wenye ulemavu.

Aidha, miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa ni kuongeza umri wa watoto wanaotambuliwa kama wategemezi kutoka miaka 21 hadi 25, hatua inayolenga kuendana na mahitaji ya familia na mazingira ya sasa.

Naye Wakili wa Mahakama Kuu na mwanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Ferdinand Makole, amesema marekebisho ya sheria yanaweza kuwa fursa muhimu ya kuongeza urahisi, ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa na NHIF.

Amesema sheria inapaswa kuweka mazingira yatakayowezesha Mfuko kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wanachama na wananchi kwa ujumla, huku ikizingatia uendelevu wa Mfuko.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Bohari ya Dawa (MSD), Brighton Mtigani, amesema ushirikishwaji wa wananchi na wadau mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha sheria inayoandaliwa inaendana na mahitaji yanayobadilika ya jamii.

Amesema ushirikishwaji huo utasaidia kujenga mfumo unaozingatia usawa katika upatikanaji wa huduma za afya na kuhakikisha makundi mbalimbali yanapata huduma bila vikwazo visivyokuwa vya lazima.

Maoni ya wadau kuchangia maboresho ya rasimu

Naye Ofisa Sheria Mwandamizi kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Japhes Daudi, amesema maoni yaliyotolewa na wadau yamechukuliwa na yataendelea kutumika katika kuboresha rasimu ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Kwa ujumla, mchakato huo unalenga kuhakikisha Sheria ya NHIF inaendana na mazingira ya sasa ya utoaji wa huduma za afya na mwelekeo wa Serikali wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kupitia mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote.

Marekebisho hayo yanatarajiwa kupanua wigo wa wananchi wanaoweza kunufaika na bima ya afya, kuimarisha udhibiti wa matumizi ya Mfuko, kuboresha huduma kwa wanachama na kuimarisha uendelevu wa NHIF, sambamba na kuchangia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote nchini.

 

*Bima ya Afya kwa Wote, Jiunge sasa*

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »