Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Viongozi wapya wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) wameapishwa rasmi jijini Dar es Salaam, huku wakitakiwa kusimamia Katiba ya chama, kulinda maslahi ya wanachama na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwajibikaji na mshikamano.
Uapisho huo umefanyika leo, Agosti 26, 2026, katika hafla iliyowakutanisha viongozi wa chama, wanachama pamoja na wageni mbalimbali, ikiwa ni hatua muhimu ya kuanza rasmi kwa kipindi kipya cha uongozi wa TAPSEA.
Akizungumza wakati wa kuwaapisha viongozi hao, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Franco Kiswaga, aliwataka viongozi hao kuzingatia Katiba ya TAPSEA na kuitumia kama msingi wa kuwaongoza wanachama pamoja na kufanya maamuzi yenye maslahi kwa chama.
Mhe. Kiswaga amesema uongozi wa chama unahitaji umakini, hekima na uwezo wa kusimamia tofauti zinazoweza kujitokeza miongoni mwa wanachama, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuhakikisha changamoto zinatatuliwa kwa kufuata Katiba na taratibu zilizowekwa.
Amesema TAPSEA ni chama kikubwa chenye wajibu wa kuwatumikia wanachama wake, hivyo viongozi wapya wanapaswa kuwa imara katika kutetea na kusimamia maslahi yao, huku wakihakikisha chama kinaendelea kukua na kufikia malengo yaliyowekwa.
“Niwaombe viongozi mnapotoka hapa mkasimamie vyema Katiba yenu ili kuweza kuondoa migogoro itakayojitokeza,” amesema Kiswaga.
Aidha, Mhe. Kiswaga amewataka viongozi hao kuwa mfano kwa wanachama katika utekelezaji wa majukumu yao, akieleza kuwa uongozi bora hujengwa kupitia uwazi, ushirikishwaji na kuheshimu taratibu zinazokubalika ndani ya chama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa TAPSEA, Leah Mwamba, amewashukuru wanachama kwa kumpa dhamana ya kuwaongoza na kuahidi kufanya kazi kwa kushirikiana nao ili kuhakikisha chama kinafikia malengo yake.
Mwamba amesema tukio la uapisho ni hatua muhimu katika safari ya uongozi wa TAPSEA na kwamba dhamana waliyopewa viongozi hao inahitaji ushirikiano wa wanachama pamoja na wadau mbalimbali.
“Ninatoa shukrani zangu za pekee kwa wote walioungana nasi katika historia hii. Jambo hili la uapisho ni kubwa sana, hivyo tunaomba mzidi kutuombea tufanye vyema katika uongozi,” amesema Mwamba.
Amesema uongozi mpya utaendelea kusikiliza maoni ya wanachama na kutafuta njia zitakazosaidia kuimarisha umoja, mshikamano na maendeleo ya chama, huku ukizingatia majukumu na wajibu uliowekwa kupitia Katiba ya TAPSEA.
Naye Katibu Mkuu wa TAPSEA, Hellen Magati, amewashukuru wageni na wadau waliohudhuria hafla hiyo, akiahidi kuwa uongozi mpya utashirikiana na wanachama katika kutekeleza majukumu yake.
Magati amesema ushirikiano wa viongozi na wanachama ni muhimu katika kuhakikisha mipango ya chama inatekelezwa kwa ufanisi na changamoto zinazojitokeza zinapata ufumbuzi kwa wakati.
Amesisitiza kuwa uongozi mpya utazingatia misingi ya ushirikiano katika kuendeleza shughuli za TAPSEA na kuhakikisha wanachama wanapata nafasi ya kutoa maoni na kushiriki katika masuala yanayohusu maendeleo ya chama.
Viongozi wengine walioapishwa ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Halima Twaha Mgulo, Makamu Mwenyekiti, Zainab Ibrahim Ally, Mweka Hazina, Nyanza Msongela, pamoja na wajumbe wengine waliochaguliwa katika uongozi huo.
Uapisho huo unatajwa kuwa hatua ya kukamilisha mchakato wa uchaguzi na kuweka rasmi uongozi mpya katika nafasi zao za kuwahudumia wanachama, huku matarajio yakiwa ni kuona chama kinaendelea kuimarisha umoja na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Viongozi hao walioapishwa leo, Agosti 26, 2026, walichaguliwa katika Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Ngurdoto, mkoani Arusha.
EmoticonEmoticon