NMB: ELIMU, UJUZI NGUZO MUHIMU YA UCHUMI WA KIPATO CHA JUU

August 25, 2026

Na Oscar Assenga, TANGA

BENKI ya NMB imesema Tanzania haiwezi kufikia uchumi wa kipato cha juu bila kuwekeza katika elimu, ujuzi wa vitendo na ubunifu unaowawezesha Watanzania kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili nchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Meneja Mwandamizi wa Maabara ya Ubunifu ya NMB, Maria Mwamyalla, wakati akitoa salamu za wadhamini kwa niaba ya wadhamini wote katika maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yaliyofanyika mkoani Tanga.

Mwamyalla alisema kaulimbiu ya mwaka huu, “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” inaendana na mkakati wa NMB wa kuwekeza katika teknolojia, ubunifu, vijana na ujumuishaji wa kifedha.

Alisema kupitia Agenda 2030, benki hiyo imeweka teknolojia, ubunifu, uwekezaji kwa vijana na ujumuishaji wa kifedha kuwa sehemu muhimu ya mkakati wake wa ukuaji.

“Mwelekeo huo unaendana moja kwa moja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi wa ushindani unaotumia maarifa, ujuzi na teknolojia,” alisema.

Mwamyalla alisema teknolojia pekee haiwezi kuleta matokeo yanayotarajiwa bila kuwapo kwa watu wenye maarifa na ujuzi wa kuitumia ipasavyo.

NMB YATOA BILIONI 2 KUSOMESHA VIJANA

Alisema kupitia NMB Foundation, benki hiyo imeendelea kuwekeza katika elimu na malezi ya uongozi kwa vijana, hususan wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi.

Alisema kupitia programu ya Nuru Yangu Scholarship and Mentorship, NMB imewekeza zaidi ya Sh bilioni mbili tangu mwaka 2022, kwa ajili ya kuwafadhili wanafunzi 121 katika vyuo vikuu 11 nchini.

Kwa mujibu wa Mwamyalla, wanafunzi hao wamekuwa wakisaidiwa mahitaji mbalimbali yakiwamo ada, malazi na vitendea kazi kama kompyuta mpakato.

Alisema wanafunzi 21 tayari wameingia katika soko la ajira, huku wengine 42 wakitarajiwa kuhitimu mwaka huu.


“Tunatarajia kufungua dirisha la tatu la programu hii mwezi Septemba mwaka huu,” alisema.

WATAKA VIJANA WAPEWE UJUZI

Aidha, Mwamyalla alisema NMB inaendelea kutekeleza programu ya SEP kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Save the Children pamoja na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Alisema programu hiyo inalenga kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa kuwapatia vijana elimu ya vitendo katika maeneo mbalimbali, ikiwamo mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na vyuo vya VETA.

NMB YAWEKEZA BILIONI 232 TEKNOLOJIA

Katika eneo la teknolojia na ubunifu, Mwamyalla alisema NMB imewekeza zaidi ya Sh bilioni 232, huku sehemu kubwa ya suluhisho za kiteknolojia zikitengenezwa na wataalamu wazawa.

Alisema uwekezaji huo unalenga kujenga utaalamu wa Watanzania, kuimarisha usalama wa mifumo pamoja na kupunguza muda wa kupeleka bidhaa za kidijitali sokoni.

Alitaja miongoni mwa suluhisho hizo kuwa ni huduma ya NMB Mkononi, inayowawezesha wateja kupata huduma mbalimbali za kibenki kupitia simu zao za mkononi, ikiwamo kutuma na kupokea malipo ya kielektroniki.

Kwa mujibu wa Mwamyalla, huduma hizo zimechangia kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha kwa zaidi ya wateja milioni 10 wa NMB.

Alisema kupitia programu ya PesaTek, iliyoanzishwa mwaka 2022, benki hiyo imezindua Innovation Sandbox na kuendelea kuwawezesha vijana pamoja na wabunifu katika sekta ya teknolojia kupima na kuendeleza suluhisho zao.

Mwamyalla alisema NMB itaendelea kushirikiana na Serikali na taasisi za elimu kuhakikisha elimu, ujuzi na ubunifu vinageuzwa kuwa suluhisho zinazochochea biashara na kuchangia maendeleo ya Taifa.


Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »