MICHEZO NI CHACHU YA AFYA,MSHIKAMANO KWA WATUMISHI-TARIMO

August 29, 2026

 MICHE



Na Mwandishi wetu- Dar es Salaam 


Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Petroli wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mha.Bruno Tarimo, amewahimiza watumishi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha afya, kuongeza mshikamano na kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na kukaa muda mrefu ofisini.


Tarimo ametoa rai hiyo leo, Agosti 29, 2026, wakati wa Bonanza la Watumishi wa PBPA lililofanyika katika viwanja vya Tanzanite Hub, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

“Tunatumia muda mwingi kutekeleza majukumu yetu tukiwa ofisini. Tunapopata nafasi kama hii ya kukutana na kufanya mazoezi kwa pamoja, tunajenga afya zetu na wakati huo huo tunahamasishana kuendelea kufanya mazoezi hata tukiwa wenyewe,” amesema Tarimo.

Ameeleza kuwa mikusanyiko ya aina hiyo pia inawapa watumishi nafasi ya kufahamiana zaidi nje ya majukumu yao ya kila siku, kujenga mahusiano mazuri na kuimarisha ushirikiano unaohitajika katika utekelezaji wa majukumu ya Wakala.


Katika bonanza hilo, watumishi walionesha ushindani na vipaji katika michezo mbalimbali ikiwemo Mpira wa Miguu, Netball, Kuvuta Kamba,Mbio za Magunia,Volleyball, Mbio za Mayai, Basketball, Kukamata kuku, Bao,Draft, Chess, Karata na Pool table.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Michezo PBPA ambaye pia ni Afisa Ubora wa Mafuta, Bw.Mosses Nyaronga, amesema mwitikio mkubwa wa watumishi katika bonanza hilo umeonesha umuhimu wa kuendelea kutoa nafasi kwa shughuli za michezo ndani ya taasisi.

“Tunawashukuru viongozi wetu kwa kutupa kibali na kutuwezesha kuandaa bonanza hili. Lengo letu ni kuhakikisha tunajenga afya zetu kupitia michezo, na tunafurahi kuona watumishi wengi wamejitokeza kushiriki,” amesema Nyaronga.

Nyaronga ametoa wito kwa viongozi wa taasisi kuendelea kuunga mkono shughuli za michezo kwa watumishi na kuwezesha mabonanza ya aina hiyo kufanyika mara kwa mara, akipendekeza yafanyike angalau kila baada ya mwezi mmoja au miwili.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »