Na Oscar Assenga, TANGA
IMAGINE umefua nguo zako, ukaondoka nyumbani kwa ajili ya shughuli zako, ghafla mvua ikaanza kunyesha. Badala ya kukimbia kurudi kuzianua, nyumba yenye teknolojia maalumu inagundua mvua na kuhamisha nguo hizo sehemu salama.
Hiyo ni moja ya bunifu zilizobuniwa na vijana wanaoshiriki katika mradi wa Vijana Bunifu, unaotekelezwa chini ya programu ya Tanga Yetu, kwa lengo la kuwajengea watoto na vijana uwezo wa kutumia Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha ya kila siku.
Bunifu hiyo imeibua matumaini mapya kwamba teknolojia inaweza kutumika kutatua hata changamoto ndogo zinazoonekana kuwa za kawaida katika maisha ya kila siku, huku ikiwapa vijana nafasi ya kugeuza mawazo yao kuwa suluhisho zinazoweza kutumika na jamii.
Akizungumza kuhusu bunifu hiyo, Mohamed Mohamed, Mkufunzi wa Masomo ya STEM kutoka Project Inspire, alisema mfumo huo umeundwa kwa kuweka kihisi (sensor) kinachoweza kutambua uwepo wa mvua.
Alisema mvua inapoanza kunyesha, kihisi hutuma taarifa kwenye mfumo na kusababisha sehemu maalumu ya kukaushia nguo kuhamia upande ambao haujanyeshewa, hivyo kuzuia nguo kulowana.
“Tumewafundisha wanafunzi namna ya kutumia teknolojia kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku. Kwa mfano, mtu amefua nguo na anatakiwa kwenda kwenye kikao, lakini mvua inaanza kunyesha. Mfumo huu unatambua mvua na kupeleka nguo sehemu ambayo hazitanyeshewa,” alisema Mohamed.
Alisema mvua inapokatika, mfumo huo hutambua mabadiliko hayo na kuirudisha sehemu ya kukaushia nguo upande wenye jua ili nguo ziendelee kukauka.
Kwa Mohamed, bunifu hiyo ni mfano wa namna vijana wanavyoweza kuangalia changamoto zinazowazunguka, kuzitafakari na kutumia maarifa ya STEM kutengeneza suluhisho badala ya kusubiri majibu kutoka kwa wengine.
Vijana wafundishwa kugeuza mawazo kuwa suluhisho
Alisema lengo la mradi wa Vijana Bunifu si kuwafundisha vijana nadharia pekee, bali kuwapa uwezo wa kuunganisha elimu wanayopata darasani na changamoto halisi zilizopo katika jamii.
“Tunataka mtoto na kijana apate interest katika masomo ya STEM, kisha aweze kuchukua wazo lililopo kichwani na kulipeleka kwenye uhalisia ili liweze kutatua changamoto katika jamii,” alisema.
Alisema Project Inspire inatekeleza mpango huo kupitia mfumo unaoitwa STEM Career Radar, unaolenga kumjengea mtoto msingi wa elimu ya STEM tangu akiwa mdogo na kumwandaa kwa taaluma mbalimbali za baadaye, zikiwamo udaktari, uhandisi na Sayansi ya Kompyuta.
Kwa mujibu wa Mohamed, programu hiyo inawahusisha watoto wenye umri wa chini ya miaka mitatu hadi 12, ambao hufundishwa sayansi kwa njia ya vitendo ili kufanya ujifunzaji kuwa rahisi, wa kuvutia na wenye matokeo.
Boot Camp chachu ya ubunifu
Alisema kwa vijana wenye umri wa miaka 13 hadi 18, mradi huo unalenga zaidi kuwawezesha kuibua na kukuza mawazo ya kibunifu yanayoweza kutatua changamoto za jamii.
Vijana hao hupewa mafunzo ya vitendo kupitia programu mbalimbali, ikiwemo Boot Camp, inayowapa nafasi ya kujifunza, kujadiliana na kuendeleza mawazo yao hadi kufikia hatua ya kutengeneza bunifu.
“Katika ngazi hii tunawawezesha vijana kujifunza kwa vitendo na kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii. Tunatumia programu mbalimbali, ikiwemo Boot Camp, ambapo vijana hupewa nafasi ya kukuza mawazo yao na kuyafanyia kazi,” alisema.
Kutoka mwanafunzi hadi kuwa mlezi wa wabunifu
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Mboni Zahoro, alisema safari yake katika STEM ilianza akiwa mwanafunzi na mshiriki wa programu ya Boot Camp, kabla ya baadaye kuamua kutumia uzoefu alioupata kuwasaidia vijana wengine.
Alisema baada ya kumaliza mafunzo, aliamua kujitolea na kujifunza zaidi namna ya kuwawezesha vijana kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu katika kutatua changamoto zinazowazunguka.
Mboni alisema kupitia mradi wa Vijana Bunifu, alipata nafasi ya kuwa STEM Communicator, jukumu linalompa nafasi ya kuwasaidia vijana wengine kukuza mawazo yao na kuyabadilisha kuwa bunifu.
“Nilianza kama mwanafunzi na mshiriki wa Boot Camp, lakini baada ya kumaliza masomo niliamua kujitolea kuwasaidia vijana wenzangu. Sasa ninawasaidia kuchukua mawazo yao na kuyakuza kupitia teknolojia na ubunifu,” alisema.
Alisema uzoefu huo umemfundisha kuwa vijana wanapopewa nafasi, vifaa na mazingira sahihi ya kujifunza, wana uwezo mkubwa wa kuibua mawazo yanayoweza kuleta mabadiliko katika jamii.
Kwa mtazamo wake, kuwafundisha vijana STEM kwa vitendo ni muhimu kwa sababu kunawapa nafasi ya kujaribu mawazo yao, kujifunza kutokana na makosa na hatimaye kutengeneza suluhisho zinazoweza kutumika katika maisha halisi.
Mradi wa Vijana Bunifu unaendelea kuonyesha kwamba ubunifu hauanzi katika maabara kubwa pekee; unaweza kuanzia kwenye changamoto ndogo inayomkabili mtoto au kijana nyumbani, shuleni au katika jamii yake—na kugeuka kuwa teknolojia yenye uwezo wa kurahisisha maisha ya watu.
EmoticonEmoticon