Na. OWM (KAM) Mwanga
Serikali imezitaka taasisi na viongozi wa dini nchini kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri maadili mema, mshikamano na uvumilivu ili kujenga jamii yenye amani, utulivu na uchaji wa Mungu.
Wito huo umetolewa leo, Agosti 30, 2026, na Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Dkt. Evaline Munisi, alipokuwa akizungumza kwenye ibada ya kumwingiza kazini Katibu Mkuu na Mtunza Hazina wa Dayosisi ya Mwanga, iliyoenda sambamba na ubarikio wa wachungaji na uingizaji kazini wa Mwinjilisti.
Dkt. Munisi ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za dini katika malezi, kuimarisha maadili ya Taifa, pamoja na kutoa huduma za kijamii kama elimu na afya.
“Taasisi za dini ni wadau muhimu wa maendeleo. Zimekuwa zikifanya kazi kubwa ya kuhamasisha wananchi kuwa wazalendo, kulinda amani na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesema Naibu Waziri huyo.
Akiwasilisha salamu za kitaifa kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Deus Sangu, Dkt. Munisi amesisitiza kuwa Serikali itaendeleza ushirikiano wa karibu na viongozi hao ili kuleta maendeleo endelevu.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amewakumbusha viongozi na watumishi wa umma pamoja na wa dini kuhusu msingi wa uongozi bora, akieleza kuwa cheo ni wito wa utumishi na wala si jukwaa la kujinufaisha.
“Uongozi wa kweli unahitaji uaminifu, unyenyekevu, uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa au matumizi mabaya ya madaraka. Viongozi wanapaswa kuwa na uchaji wa Mungu na uwezo wa kuwatumikia wananchi kwa haki,” amesisitiza Dkt. Munisi.
Amewataka viongozi na watumishi wapya waliosimikwa katika ibada hiyo kuongoza waumini kwa hekima na upendo, huku wakidumisha misingi ya amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Akizungumza awali Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mwanga Dkt. Daniel Mono ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi , Ajira na Mahusiano kwa kuitikia wito wa mwaliko wa kushiriki ibada maalumu ya kumwingiza kazini Katibu Mkuu na Mtunza Hazina wa Dayosisi na tukio la Ubarikio wa Wachungaji na Kumwingiza kazini Mwinjilisti, jambo ambalo linaonyesha mahusiano mazuri ya Serikali na taasisi za kidini.
Askofu Mono ameongeza kuwa Mahusiano mazuri ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini katika kuwahudumia wananchi.









EmoticonEmoticon