Na Abduly Madenge, WAF – Dar es Salaam
Tanzania imeandika historia mpya katika sekta ya afya baada ya wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufanikisha kwa mara ya kwanza upasuaji wa kupandikiza mashine za usikivu (Cochlear Implant) kwa kutumia wataalamu wa ndani pekee, bila kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi.
Mafanikio hayo yameelezwa kuwa hatua kubwa ya kuimarisha huduma za ubingwa bobezi nchini, kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za afya za kibingwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza Julai 28, 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakati wa hafla ya kuwasha mashine 13 za usikivu kwa watoto saba waliofanyiwa upasuaji mwezi Juni mwaka huu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Bw. Emmanuel Tayari, amesema mafanikio hayo yanaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuendelea kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata matibabu ya kisasa ndani ya nchi.
Amesema tatizo la ulemavu wa usikivu bado ni changamoto kubwa nchini, ambapo takribani watoto 12,000 huzaliwa au hupata ulemavu mkubwa wa usikivu kila mwaka. Kutokana na hali hiyo, Serikali imeendelea kuwekeza katika huduma za kinga, uchunguzi wa mapema, matibabu pamoja na huduma za urekebishaji ili kuwasaidia watoto hao kupata fursa sawa za maendeleo.
Bw. Tayari amesema tangu mwaka 2017, Hospitali ya Taifa Muhimbili imefanikiwa kufanya upasuaji wa Cochlear Implant kwa wagonjwa 115, hatua iliyosaidia kupunguza utegemezi wa matibabu ya nje ya nchi na kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo awali zilitumika kuwapeleka wagonjwa kupata huduma hizo nje ya Tanzania.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika kuendeleza rasilimali watu katika sekta ya afya kupitia mpango wa Dr. Samia Scholarship, ambao hadi sasa umenufaisha watumishi 6,169.
Kupitia mpango huo, wataalamu wa magonjwa ya masikio, pua na koo wamepata mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi ndani na nje ya nchi, hatua iliyowezesha kujengwa kwa uwezo wa ndani wa kutoa huduma hizo.
Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) imeanzisha programu za Shahada ya Sayansi katika Elimu ya Usikivu pamoja na Tiba ya Usemi na Lugha, zikiwa na lengo la kuongeza idadi ya wataalamu wa huduma za usikivu na kuimarisha huduma hizo katika ngazi zote za utoaji huduma nchini.
Bw. Tayari amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kugharamia huduma za kibingwa, kusomesha wataalamu zaidi na kuimarisha uwezo wa hospitali za rufaa za mikoa, kanda na taifa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo wanayoishi, huku ikipunguza kwa kiwango kikubwa rufaa za matibabu nje ya nchi.
Mafanikio ya upasuaji wa Cochlear Implant kwa kutumia wataalamu wa ndani yanaonesha hatua kubwa ambayo Tanzania imefikia katika safari ya kujenga mfumo imara wa afya unaojitosheleza kwa wataalamu, teknolojia na huduma za kisasa zinazokidhi mahitaji ya wananchi.










EmoticonEmoticon