WAZIRI SANGU: MSHIKAMANO NA AMANI NDIO NGUZO YA MAENDELEO YA TAIFA

June 13, 2026
Na: OWM-KAM, Mwanza

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano, umoja na amani kwa kuwa ni nguzo muhimu zinazowezesha taifa kufikia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 13, 2026 Jijini Mwanza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, alipomwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika hafla ya kumsimika Askofu Mkuu wa Nne wa Kanisa la Tanzania Missionary Revival Church (TMRC), Askofu Stephano Ngulimi Saguda.

Mhe. Sangu amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za dini kwa kuwa ni wadau muhimu katika kudumisha amani, kukuza maadili na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Amesema falsafa ya Uwazi, Ushirikiano na Maridhiano inayotekelezwa na Rais Samia imeendelea kuimarisha umoja wa Watanzania na kuwajumuisha wadau mbalimbali katika juhudi za kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Aidha, Mhe. Sangu amelipongeza Kanisa la TMRC kwa mchango wake mkubwa katika kueneza Injili, kukuza maadili mema, kuimarisha ushirikiano wa kidini pamoja na kutoa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo huduma za afya kupitia Kituo cha Afya cha TMRC Urafiki.

Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za dini katika kujenga jamii yenye maadili, ustahimilivu na mshikamano, huku akizitaka taasisi hizo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii.

Katika hafla hiyo, Mhe. Sangu amempongeza Askofu Mkuu mpya wa TMRC, Askofu Stephano Ngulimi Saguda, kwa kuaminiwa kuongoza kanisa hilo, akieleza kuwa Serikali ina imani kuwa chini ya uongozi wake kanisa litaendelea kuwa chombo muhimu cha kuhubiri amani, upendo na maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa TMRC, Stephano Ngulimi Saguda, amewataka waumini wa kanisa hilo kuendelea kuliombea Taifa, kuheshimu mamlaka zilizopo madarakani na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ili kuimarisha mshikamano na amani nchini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng’wilabuzu Ndatwa Ludigija, amesema viongozi wa dini wamekuwa daraja muhimu katika kufikisha ujumbe wa Serikali kwa wananchi na kuhamasisha mshikamano, maadili na uwajibikaji katika jamii.

Mhe. Sangu amehitimisha kwa kuwataka Watanzania kuendelea kulinda na kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, akisisitiza kuwa msingi huo ndiyo nguzo kuu ya maendeleo endelevu ya Taifa na urithi muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »