SERIKALI YASISITIZA NAFASI YA UTAFITI KATIKA KUJENGA UCHUMI WA MAARIFA

June 11, 2026
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Serikali imesisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu, utafiti na ubunifu kama nguzo muhimu za kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, teknolojia na ushindani wa kimataifa.

Msisitizo huo umetolewa leo Juni 11, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, alipomwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, katika hafla ya kufunga rasmi Maadhimisho ya Kumi na Moja ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Dkt. Nungu amesema mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yatategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa mfumo wa elimu kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kisasa, maadili mema, uwezo wa kubuni teknolojia na kutatua changamoto zinazolikabili taifa.

Amesema Serikali inaendelea kuimarisha sekta ya elimu kupitia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023, inayosisitiza elimu jumuishi, matumizi ya TEHAMA, ujifunzaji unaozingatia umahiri na mafunzo kwa vitendo ili kuwajengea wahitimu uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira.

“Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga Tanzania yenye uchumi imara, jumuishi na unaoongozwa na maarifa. Hivyo, vyuo vikuu vina wajibu wa kuendelea kuzalisha maarifa, tafiti na ubunifu unaochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesema.

Alieleza kuwa UDSM imeendelea kuwa miongoni mwa taasisi muhimu zinazochangia maendeleo ya taifa kupitia tafiti na ubunifu katika sekta mbalimbali ikiwemo madini, nishati, uhandisi, mifumo ya kidijitali, usalama wa taarifa, mazingira, uchumi na sera za maendeleo.

Dkt. Nungu pia ameipongeza UDSM kwa kuendelea kuongoza katika elimu ya juu nchini na kwa mchango wake katika kutoa ushauri wa kitaalamu, kufanya tafiti zenye tija na kuendeleza ubunifu unaosaidia kutatua changamoto za maendeleo.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti, Prof. Nelson Boniface, amesema maadhimisho ya mwaka huu yameonyesha kukua kwa utamaduni wa utafiti na ubunifu ndani ya chuo hicho.

Amesema jumla ya miradi 318 iliwasilishwa katika ngazi ya idara kati ya Mei 19 na Juni 4, mwaka huu, ambapo miradi 210 sawa na asilimia 66 iliwasilishwa na wanafunzi huku miradi 108 sawa na asilimia 34 ikitoka kwa wafanyakazi wa chuo.

Prof. Boniface amesema baada ya mchakato wa tathmini, miradi 106 bora ilichaguliwa kushiriki katika maonesho ya ngazi ya chuo. Kati ya hiyo, miradi 26 ilitoka kwa wanafunzi wa shahada za awali na uzamili, huku miradi 80 ikihusu maeneo ya utafiti, ubunifu, ushirikiano, ushauri elekezi na mabadiliko ya kimkakati.

Amesema takwimu hizo zinaashiria mafanikio ya juhudi za chuo katika kuhamasisha ushiriki wa wanafunzi na watafiti katika uzalishaji wa maarifa, teknolojia na suluhisho bunifu kwa maendeleo ya jamii.

Aidha, amesema maadhimisho hayo yalivutia washiriki takribani 680 kutoka sekta mbalimbali, wakiwemo watafiti, wafanyabiashara, watunga sera, wanafunzi na wananchi.

“Ushiriki huu unaonesha kuwa Wiki ya Utafiti na Ubunifu imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha maarifa, ubunifu, sekta binafsi na jamii kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya taifa,” amesema.

Ameongeza kuwa maadhimisho hayo yameendelea kufungua fursa za kiuchumi kwa washiriki kupitia maonesho ya bidhaa, huduma na teknolojia mbalimbali zilizotokana na tafiti na ubunifu.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »