Farida Mangube Morogoro
Juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na changamoto za upatikanaji wa maji zimepata msukumo mpya kufuatia kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya watafiti na jamii kupitia mradi wa kimataifa wa ICP Connect na Lab to Life.
Hatua hiyo imebainishwa wakati wa semina ya kuwasilisha matokeo ya awali ya tafiti za sayansi ya jamii iliyofanyika Chuo Kikuu Mzumbe Kampas kuu Morogoro, ikiwa ni sehemu ya awamu ya pili ya mradi huo.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa kimataifa unaojumuisha Chuo Kikuu cha Antwerp (Ubelgiji), Chuo Kikuu Mzumbe, Taasisi ya Sera ya Maendeleo (IOB), Chuo Kikuu cha Kikristo cha Uganda (UCU), pamoja na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika ya Nelson Mandela (NM-AIST), Arusha.
Akifungua semina hiyo, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Utafiti na Ushauri), Dkt. Proscovia Kamugisha, alisema mradi huo umeongeza uwezo wa kitaifa katika ufuatiliaji na tathmini ya maendeleo kupitia programu ya Shahada ya Uzamili ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Maendeleo (MDME).
Alisisitiza kuwa kuunganisha utafiti na jamii ni hatua muhimu katika kuhakikisha tafiti zinatoa matokeo yenye tija kwa maendeleo ya wananchi.
“Lengo letu ni kuhakikisha matokeo ya tafiti hayabaki kwenye makabrasha, bali yanawafikia na kuwasaidia wananchi moja kwa moja,” alisema Dkt. Kamugisha.
Kwa upande wake, Mratibu wa mradi huo, Dkt. Christina Shitima alieleza kuwa mafanikio makubwa ya mradi huo ni kuwashirikisha wananchi moja kwa moja katika tafiti. Alibainisha kuwa mbinu hiyo imeongeza uelewa wa pamoja kati ya watafiti na jamii, na kuwezesha kupatikana kwa suluhisho yanayokubalika na kudumu.
Naye Dkt. Lucy Massoi alisisitiza kuwa ushirikishwaji wa wadau unazifanya jamii kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto zao wenyewe, hatua inayochangia kuboresha sera na kuinua ustawi wa maisha ya kila siku.
Akichangia mada katika semina hiyo, Bw. Richard Temu kutoka shirika la Twaweza alieleza kuwa matumizi ya mbinu za uraghbishaji (animation) yamekuwa chachu ya mabadiliko kwa jamii. Alifafanua kuwa mbinu hizo huwabadilisha wananchi kutoka kuwa wasikilizaji wa taarifa hadi kuwa washiriki hai katika kutambua na kutatua changamoto zinazowakabili.
“Wananchi wanapopewa nafasi ya kushiriki kikamilifu, wanakuwa sehemu ya suluhisho badala ya kuwa watazamaji,” alisisitiza.
Semina hiyo iliwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu, TURUWASA Mvomero, viongozi wa kata na vijiji kutoka Tarafa ya Turiani, pamoja na watafiti, wanafunzi na wahadhiri kutoka taasisi washirika.
Katika uwasilishaji wa tafiti, wanafunzi walionesha matokeo ya kazi zao katika maeneo ya vijijini, yakitoa taswira halisi ya changamoto na suluhisho zinazotekelezeka. Katika kijiji cha Kilimanjaro, Kata ya Kisala, Tarafa ya Turiani, wilayani Mvomero, waliweka kifaa cha kisasa cha ufuatiliaji wa hali ya hewa kinachopima kasi ya upepo, unyevunyevu na mwenendo wa maji mtoni. Takwimu hizo zinasaidia kutoa tahadhari ya mapema dhidi ya mafuriko na kuongeza utayari wa jamii kukabiliana na majanga ya asili.
Katika kijiji cha Lusanga, utafiti uliofanywa ulibaini changamoto za muda mrefu za upatikanaji wa maji, ikiwemo utegemezi wa vyanzo visivyo salama, upungufu wa maji wakati wa kiangazi, pamoja na miundombinu duni. Ili kukabiliana na hali hiyo, watafiti walipendekeza kuimarishwa kwa usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji, ulipaji wa huduma kwa wakati, na matumizi ya mbinu rahisi za usafi kama kuyachemsha au kuyachuja maji kabla ya matumizi.
Mbali na matokeo ya tafiti, semina hiyo ilionesha wazi kuwa kuunganisha maarifa ya kitaaluma na uzoefu wa jamii ni msingi muhimu wa kupata suluhisho endelevu kwa changamoto za maendeleo.
Akihitimisha semina hiyo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Uchumi, Dkt. Robert Lihawa, alisema kuwa tafiti shirikishi zinapaswa kupewa kipaumbele kwani ndizo zenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya kweli kwa jamii.
“Maendeleo endelevu hayawezi kufikiwa bila ushirikiano wa karibu kati ya watafiti, jamii na watunga sera,” alisema.
Kadri athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyoendelea kuongezeka, jitihada kama hizi zinatarajiwa kuwa nguzo muhimu katika kusaidia jamii kujenga ustahimilivu na kuboresha upatikanaji wa rasilimali muhimu kama maji.





EmoticonEmoticon