Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Uchumi na Uwekezaji Zanzibar imeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya gesi asilia mkoani Mtwara.
Hayo yameelezwa Aprili 16, 2026 wakati wa ziara iliyoratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa lengo la kuongeza uelewa kwa wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi asilia.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Makame Sufiani amebainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya kazi kubwa kuwekeza katika miundombinu ya gesi asilia, hatua iliyoleta manufaa makubwa kwa Taifa.
“Tumeridhishwa na kazi kubwa inayofanyika hapa Mtwara. Huu ni mfano mzuri wa namna rasilimali za Taifa zinavyoweza kusimamiwa kwa tija na kuwanufaisha wananchi,” alisema Sufiani
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mhe. Mboja Mshenga, ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza hatua za awali za ukusanyaji data za petroli za mfumo wa 3D zitakazowezesha kubaini uwepo wa gesi asilia na mafuta visiwani humo.
“Tumeanza hatua za msingi za utafiti ili kufungua fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, jambo litakalosaidia kukuza uchumi wa Zanzibar na kuongeza mapato ya Serikali,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PURA, Ndg. Halfani Halfani, amesema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Hati ya Mashirikiano iliyoingiwa kati ya PURA na Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta Zanzibar (ZPRA) mwaka 2022.
Ameeleza ushirikiano huo unawapa fursa ya kubadilishana uzoefu wa kiufundi na kitaalamu katika usimamizi na udhibiti wa shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji mafuta na gesi asilia.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi wa sekta hiyo na kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinatumika kwa manufaa ya wananchi.






EmoticonEmoticon