FEDHA ZA CSR ZA BARRICK BULYANHULU KUENDELEA KULETA MAENDELEO HALMASHAURI YA WILAYA YA NYANG’HWALE

April 12, 2026

Meneja wa Mahusiano ya Jamii na Mazingira wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu , Bw Agapiti Paul (kushoto) akibadilishana mkataba wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia (CSR) Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, John Isack (kulia) wengine pichani ni maofisa waandamizi wa halmashauri hiyo.
Meneja wa Mahusiano ya Jamii na Mazingira wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu , Bw. Agapiti Paul akiongea katika hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia (CSR) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, John Isack akiongea katika hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia (CSR) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Meneja wa Mahusiano ya Jamii na Mazingira wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu , Bw Agapiti Paul akisaini mkataba.

#Mgodi kutoa shilingi milioni 900 kwa utekelezaji wa miradi ya mwaka huu

Uwekezaji wa kampuni ya Barrick nchini yenye ubia Serikali nchini kupitia kampuni ya Twiga unazidi kuleta manufaa kwa wananchi ambapo mgodi wa Barrick Bulyanhulu uliopo wilayani Msalala na Nyang’hwale umesaini mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale ambapo katika kipindi cha mwaka huu utatoa kiasi cha shilingi milioni 900 za uwajibikaji kwa jamii (CSR) kwa ajili ya kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hafla ya kusaini mkataba huo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Wafanyakazi wa Barrick Bulyanhulu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nyang’hwale, John Isack John, akiongea katika hafla hiyo amesema kuwa fedha hizo zitawezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali 9 katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, fedha, utawala,maendeleo ya jamii, mali asili na uhifadhi wa mazingira.

Ameitaja miradi itakayotekelezwa kuwa ni ujenzi wa soko la dhahabu (awamu ya kwanza),ufugaji wa nyuki katika msitu wa Miyenze,ujenzi wa nyumba ya mtumishi na uchimbaji wa kisima katika shule ya sekondari Iyenze pamoja na ununuzi wa vitanda 240 kwa mabweni ya shule za sekodari za Bukwimba, Busolwa na Kenegele.

Aidha, miradi mingine ni pamoja na ununuzi wa madawati na samani za walimu katika Shule Mpya ya Msingi Sengerema, ukamilishaji wa miundombinu ya maji na umeme katika Zahanati ya Mwabui, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA kwa watendaji wa vijiji na kata ya Mwingiro, pamoja na uchimbaji wa rambo la kunyweshea mifugo katika kijiji cha Ng’wasabuka.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, John Isack amesema ni muhimu miradi yote iliyopangwa kutekelezwa ikamilike kwa wakati ili iweze kuleta matokeo chanya kwa jamii husika.

“Tunataka miradi hii hasa ya elimu kama ni madawati , vitanda , ujenzi wa mabweni na nyumba za watumishi katika sekta ya elimu zikamilike kwa wakati na muda uliopagwa,” amesema Isack.

Ametoa wito kwa madiwani na Watalamu wa Halmashauri hiyo kuwatangazia wananchi miradi hii inayotekelezwa na fedha za uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka mgodi wa Barrick Bulyanhulu, ili wafahamu umuhimu wa kuwepo mgodi huu katika eneo lao.

Kuhusiana na ufanisi wa miradi inayotekelezwa na fedha za CSR kutoka Barrick Bulyanhulu, Isack amesema ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya CSR katika wilaya hiyo umekuwa ukizidi kuwa bora mwaka hadi mwaka na kwa sehemu kubwa utajikita kwenye miradi ya kijamii ambayo ni vipaumbele vya wananchi wa maeneo husika.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Barrick katika hafla hiyo ambaye ni Meneja wa Mahusiano ya Jamii na Mazingira wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu , Bw. Agapiti Paul amesema fedha hizo za CSR zitatatumika kufanikisha miradi ya maendeleo kama vile elimu , afya , uboreshaji wa miundombinu na ujenzi wa nyumba za watumishi katika sekta ya elimu na afya.

“Kwa kweli mwaka huu katika miradi iliyonipa furaha na ujenzi wa soko la dhahabu hapa Nyang’hwale ambapo itakuwa ni chanzo kikuu cha uchumi na itaongeza thamani ya miradi ya kijamii na kuwa chanzo cha ukuaji wa uchumi kwa wachimbaji wadogo na vile vile ni kichocheo cha kusukuma miradi mengine ya maendeleo kama vile elimu , afya , barabara na shughuli zingine za uzalishaji mali, amesema Paul.

Amefafanua kwamba katika kuhakikisha wananchi wananufaika na uchimbaji madini, Mgodi wa Barrick utaendelea kuisaidia jamii zinazozunguka mgodi huo kwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali na barabara.

Katika kipindi cha mwaka uliopita mgodi wa Barrick Bulyanhulu ulitoa kiasi cha shilingi bilioni 1 na milioni 75 za uwajibikaji kwa jamii (CSR) ambazo zimefanikisha miradi miradi mbalimbali ya kijamii ya kuboresha maisha ya wananchi.

Meneja wa Mahusiano ya Jamii na Mazingira wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu , Bw. Agapiti Paul akiongea katika hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia (CSR) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Meneja wa Mahusiano ya Jamii na Mazingira wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu , Bw. Agapiti Paul akiongea katika hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia (CSR) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, John Isack akiongea katika hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia (CSR) katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »