NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Limerick cha nchini Ireland wamesaini hati ya makubaliano ya utekelezaji wa ufadhili wa Samia Scholarship Extended, utakaowawezesha wanafunzi 32 kusoma katika chuo hicho.
Makubaliano hayo yamesainiwa leo Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam, yakishuhudiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda pamoja na ujumbe kutoka ubalozi wa Ireland nchini na viongozi wa chuo hicho.
Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Mkenda amesema ufadhili huo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha elimu kwa kuandaa wataalamu wa sayansi na teknolojia watakaoendana na mahitaji ya dunia ya sasa.
Amesema ushirikiano huo umefanyika wakati muafaka ambapo Tanzania inaendelea kujenga uchumi unaotegemea maarifa na ubunifu, huku ukilenga kuwawezesha vijana kupata elimu bora, uzoefu wa kimataifa na ujuzi wa kisasa.
Aidha, chuo hicho kimetoa punguzo la ada kwa asilimia 50 kwa wanafunzi watakaojiunga kupitia mpango huo.
Profesa Mkenda alibainisha kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa Samia Scholarship katika fani za Sayansi ya Data, Akili Unde (AI) na taaluma zinazohusiana, ikiwa ni mkakati wa kuwajengea vijana uwezo katika teknolojia mpya.
“Tayari tumewapeleka wanafunzi 34 nchini Ireland, ambapo 32 wanasoma katika Chuo Kikuu cha Limerick na wawili katika Chuo cha Cork,” amesema.
Ameongeza kuwa wanafunzi hao ni sehemu ya ufadhili wa wanafunzi 50 waliofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita, huku wengine 16 wakiwa tayari wamejiunga na vyuo vikuu nchini Afrika Kusini.
Kwa upande wake, Balozi wa Ireland nchini, Nicola Brennan, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu bora ili kukidhi mahitaji ya ajira kwa idadi kubwa ya vijana inayotarajiwa kuongezeka kufikia mwaka 2050.
Amesema Tanzania ina rasilimali watu yenye nguvu na mazingira ya utulivu yanayowezesha maendeleo, lakini uwekezaji mkubwa katika elimu ni muhimu ili kuendana na ongezeko la watu.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Limerick, Colin Fitzpatrick, amesema chuo hicho kinajikita katika mafunzo ya vitendo na kuwapatia wanafunzi uzoefu kupitia ushirikiano na kampuni kubwa za kimataifa.
Amesema hatua hiyo itawasaidia wanafunzi kutoka Tanzania kupata ujuzi wa nadharia na vitendo katika mazingira halisi ya kazi, hasa katika sekta ya teknolojia inayokua kwa kasi duniani.

EmoticonEmoticon