Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imepokea ugeni kutoka Chuo Kikuu cha Limerick cha nchini Ireland , ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika elimu, tafiti na ubunifu kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended Data Science and Artificial Intelligence (SSE DS/AI+).
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Naibu Makamu Mkuu wa NM-AIST anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ubunifu, Profesa Anthony Mshandete, amesema ujio wa ugeni huo umefungua fursa mpya katika maeneo ya kipaumbele, ikiwemo ubiasharishaji wa matokeo ya tafiti pamoja na kuendeleza programu za akili unde (Artificial Intelligence) na sayansi kwa ujumla, hatua itakayochochea maendeleo ya kiteknolojia nchini.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Limerick anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa na Jamii, Profesa Colin Fitzpatrick, amesema wamefurahishwa kukutana na wanafunzi wenye vipaji na viwango vya juu katika NM-AIST. Ameeleza kuwa Chuo Kikuu cha Limerick huvutia wanafunzi mahiri kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuwapa uzoefu wa kimataifa. Ameongeza kuwa ameridhishwa na maandalizi ya wanafunzi hao pamoja na mfumo bora wa ufadhili wa masomo unaowawezesha kufanikiwa katika taaluma zao.
Naye Mratibu wa Bootcamp katika NM-AIST na Mkuu wa Shule ya Biashara (BuSH), Profesa Lilian Pasape, amesema ujio wa chuo hicho ni fursa muhimu kwa wanafunzi. Amebainisha kuwa Chuo Kikuu cha Limerick ni miongoni mwa vyuo vinavyoongoza duniani kwa kuunganisha masomo na sekta ya viwanda pamoja na makampuni. Amesema kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended Data Science and Artificial Intelligence (SSE DS/AI+), wanafunzi 32 kati ya 50 wamechaguliwa kujiunga na chuo hicho, hali inayoonyesha ubora wa programu hiyo na kuongeza uwezekano wa wahitimu kupata ajira mara baada ya kuhitimu.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wanufaika wa ufadhili huo, mwanafunzi Anita Kulwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imewawezesha vijana wengi kupata elimu bora ya juu. Ameahidi kutumia ipasavyo fursa hiyo kwa kujituma katika masomo yake, hususan katika maeneo ya sayansi ya data na akili unde, ili kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kwa ujumla, ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma, kuongeza ubunifu na kuchochea maendeleo ya teknolojia nchini kupitia programu za pamoja kati ya Tanzania na Ireland.





EmoticonEmoticon