EAC YAIMARISHA MFUMO WA KURAHISISHA BIASHARA ZA MIPAKANI

July 15, 2026



Na Oscar Assenga,MKINGA

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imeeleza itaendelea kuimarisha utekelezaji wa Mfumo Rahisi wa Biashara (Simplified Trade Regime-STR) ili kurahisisha biashara za mipakani, kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kuongeza uzalishaji, kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya ukanda na kupunguza gharama za biashara.


Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Forodha, Biashara na Fedha, Annette Semuwamba, wakati alipotembelea Kituo cha Huduma cha Pamoja Mpakani (One Stop Border Post-OSBP) cha Horohoro wilayani Mkinga, mkoani Tanga.


Ziara hiyo ni sehemu ya tathmini ya utekelezaji wa Mfumo Rahisi wa Biashara katika vituo saba vya Huduma vya Pamoja Mpakani vilivyopo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Semuwamba alisema EAC itaendelea kushirikiana na nchi wanachama na wadau mbalimbali kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanaovuka mipaka wanapata mazingira rafiki kupitia taratibu rahisi za forodha.

“Tumefurahishwa kuona biashara kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inaendelea kukua. Kinachotutia moyo zaidi ni kwamba bidhaa nyingi zinazovuka mipaka ni bidhaa zinazozalishwa ndani ya ukanda wetu,” alisema.

Alisema uwekezaji uliofanywa katika miundombinu ya vituo vya Huduma vya Pamoja Mipakani umechangia kupunguza muda wa kuhudumia mizigo na wasafiri, kupunguza gharama za biashara na kusaidia kushusha bei za bidhaa kwa walaji.

Aidha, aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufunga mashine ya kisasa ya ukaguzi wa mizigo (scanner) katika mpaka wa Horohoro/Lunga Lunga, akisema hatua hiyo itaharakisha ukaguzi na uondoshaji wa mizigo.

Semuwamba alipendekeza pia kuanzishwa kwa mfumo wa kubadilishana picha za mizigo iliyokaguliwa kwa kutumia mashine hizo kati ya vituo vya Huduma vya Pamoja Mipakani ili kupunguza gharama za uwekezaji wa vifaa hivyo katika maeneo mengine ya mipakani.

Awali, Mkuu wa Kituo cha Huduma cha Pamoja Mpakani Horohoro, Shadrack Mbonea, alisema kituo hicho kimechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha biashara na usafirishaji wa mizigo kati ya Tanzania na Kenya.

Alisema Horohoro ni miongoni mwa vituo saba vya Huduma vya Pamoja Mipakani nchini vinavyowezesha wasafiri, magari na mizigo kupata huduma zote za mipakani katika eneo moja badala ya kuhudumiwa kila upande wa mpaka.

“Kituo hiki kilianza majaribio ya utoaji wa huduma kwa mfumo wa One Stop Border Post mwezi Septemba 2021 na tangu wakati huo kimeendelea kufanya kazi kwa mafanikio makubwa,” alisema.

Mbonea alisema kituo hicho kina taasisi 19 za Serikali zinazoongozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zikiwemo Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), TASAC, Tume ya Madini, Idara ya Uvuvi, Idara ya Mifugo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Alisema taasisi hizo zina jukumu la kukusanya mapato ya Serikali, kurahisisha biashara, kulinda jamii dhidi ya bidhaa hatarishi, kutekeleza sera za biashara, kukusanya takwimu za biashara za mipakani na kudhibiti magendo.

Kwa mujibu wa Mbonea, hapo awali mfumo wa OSBP ulikuwa ukifanya kazi kwa saa 12 kwa siku, hali iliyowalazimu wasafiri na wasafirishaji wa mizigo kukamilisha taratibu za forodha katika kila upande wa mpaka.

Alisema kupitia makubaliano kati ya Tanzania na Kenya, huduma sasa zinatolewa kwa saa 24, hatua iliyopunguza muda wa kusubiri na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Aidha, alisema kituo hicho kinatekeleza Mfumo Rahisi wa Biashara unaowawezesha wafanyabiashara wadogo wanaosafirisha bidhaa zenye thamani isiyozidi dola za Marekani 2,000 kutumia taratibu rahisi za forodha.

“Tumeanzisha dawati maalumu la kuwahudumia wafanyabiashara wadogo, tumerahisisha utaratibu wa ukadiriaji wa kodi kwa kutumia fomu ya F88 na tunatambua Vyeti Rahisi vya Asili ya Bidhaa vinavyotolewa na mamlaka za Kenya,” alisema.

Aliongeza kuwa kituo hicho pia kinatekeleza Mfumo wa Himaya Moja ya Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single Customs Territory-SCT), ambao umechangia kupunguza muda wa uondoshaji wa mizigo, kushusha gharama za biashara na kuondoa vikwazo vya biashara ndani ya ukanda.

Alisema ushirikiano kati ya Horohoro na Lunga Lunga umeimarisha mapambano dhidi ya magendo kupitia doria za pamoja, mikutano ya kila robo mwaka na utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu taratibu za biashara za mipakani.

Takwimu zinaonyesha kuwa thamani ya bidhaa zinazouzwa nje kupitia mpaka wa Horohoro/Lunga Lunga imeongezeka kutoka Sh milioni 306.4 mwaka wa fedha 2022/23 hadi Sh milioni 548 mwaka 2024/25. Aidha, thamani ya bidhaa zinazoingizwa nchini kupitia mpaka huo imeongezeka kutoka Sh milioni 134.7 hadi Sh milioni 175.9 katika kipindi hicho.

Ongezeko hilo linaakisi mafanikio ya juhudi za EAC na nchi wanachama katika kuimarisha biashara za mipakani, kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya ukanda na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Kenya.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »