OPERESHENI YA POLISI TANGA YANASA WATUHUMIWA 200 WENGINE 51 WAHUKUMIWA

July 17, 2026



Na Oscar Assenga, Tanga

Operesheni zilizoendeshwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kwa kipindi cha Juni 1 hadi Julai 16, 2026 zimewezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 200 wanaodaiwa kuhusika na makosa mbalimbali ya jinai, huku watuhumiwa 51 wakitiwa hatiani na mahakama na kuhukumiwa vifungo tofauti, wakiwamo wawili waliofungwa miaka 30 gerezani.

Makosa yanayowakabili watuhumiwa hao ni pamoja na unyang'anyi wa kutumia nguvu, wizi, biashara ya dawa za kulevya, kupatikana na mali zinazodhaniwa kuwa za wizi, umiliki wa nyara za Serikali, uharibifu wa miundombinu ya umma, matumizi ya noti bandia na makosa mengine ya jinai.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Muchunguzi, alisema mafanikio hayo yametokana na operesheni maalumu na doria zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Alisema kati ya watuhumiwa waliokamatwa, kesi za watu 51 zilikamilika na kufikishwa mahakamani, ambako walipatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu mbalimbali kwa makosa ya kulawiti, kubaka, kuzini na maharimu, kusafirisha dawa za kulevya, wizi wa mifugo, kuvunja na kuiba, kujeruhi, kutishia kuua, kuingia nchini bila kibali pamoja na makosa mengine.
Watatu wafungwa miaka 30

Muchunguzi alisema waliohukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani ni Julius Mustafa, aliyepatikana na hatia ya kulawiti, Kilimo Issaya aliyetiwa hatiani kwa kosa la kuzini na maharimu na Sadiki Waziri aliyepatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya.

Aliongeza kuwa watuhumiwa wengine walihukumiwa vifungo vya miaka mitano gerezani kwa makosa ya wizi wa mifugo pamoja na makosa mengine ya jinai.

Dawa za kulevya zanasa 29

Akizungumzia operesheni za kupambana na dawa za kulevya, Muchunguzi alisema watuhumiwa 29 walikamatwa wakiwa na dawa hizo za aina mbalimbali.

Alisema watuhumiwa 14 walikutwa na mabunda 750 ya mirungi yenye uzito wa kilogramu 45, huku watuhumiwa wengine 15 wakinaswa na bangi ikiwa katika mfumo wa misokoto 114, pakiti 126, vifurushi vitano na kete 120.

Katika operesheni hizo, polisi pia walikamata pikipiki 20 zisizo na namba za usajili ambazo zinaendelea kuchunguzwa kubaini uhalali wa umiliki wake na kama zilitumika kutekeleza vitendo vya uhalifu.
Nyara za Serikali, mali za wizi zakamatwa

Operesheni hizo pia zilisababisha kukamatwa kwa watuhumiwa watano waliokuwa na nyara za Serikali na mali zinazohusiana na wanyamapori.

Mbali na hilo, polisi walinasa vifaa mbalimbali vinavyodhaniwa kuwa vya wizi, vikiwamo vifaa vya miundombinu ya TANESCO, vifaa vya miundombinu ya barabara, noti bandia za fedha za Kenya, televisheni 10, simu za mkononi 25 pamoja na mali nyingine zinazochunguzwa kubaini uhalali wa umiliki wake.

Muchunguzi alisema operesheni dhidi ya uhalifu zitaendelea kuimarishwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga, huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kuwabaini wahalifu na kuzuia vitendo vya uhalifu.

Alisema ushirikiano wa wananchi umeendelea kuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya operesheni hizo na kwamba jeshi hilo litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na uhalifu.








Share this

Related Posts

Previous
Next Post »