Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini vya Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati vimekubaliana kushirikiana katika mifumo ya ufuatiliaji na kusimamia kwa pamoja tathmini ya utekelezaji wa miradi ya nishati na maji ili kuhakikisha kuwa inafanyika kwa ufanisi na hivyo kuwezesha wananchi kupata huduma bora.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Maji, Mtumba, jijini Dodoma, kikihusisha wataalam wa ufuatiliaji na tathmini kutoka wizara zote mbili.
Katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Nishati, Bi. Anitha Ishengoma, pamoja na Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Maji, Bi. Diana Kimario, wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano huo ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.
Bi. Anita Ishengoma amesema vitengo vya ufuatiliaji na tathmini vina jukumu la msingi katika kuhakikisha sera na mipango ya wizara pamoja na taasisi zake inatekelezwa ipasavyo.
“Ni muhimu kwa vitengo vya ufuatiliaji na tathmini kuhakikisha sera na mipango ya wizara na taasisi zake inatekelezwa ipasavyo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za maji na nishati kwa wananchi,” Amesema
Kwa upande wake, Bi. Kimario kutoka Wizara ya Maji, amesema Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati zimekuwa zikifanya kazi kwa ukaribu kwa muda mrefu, hasa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayogusa sekta zote mbili ukiwemo mradi wa umeme wa Julius Nyerere wa megawati 2,115 hivyo kuunganisha nguvu kwa Wizara hizo mbili kutatoa matokeo chanya zaidi katika utekelezaji wa miradi.






EmoticonEmoticon