MASHINE ZA UKAGUZI WA MIZIGO ZAKIDHI VIGEZO VYA TAEC KANDA YA ZIWA

February 12, 2026

Serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeendelea kuimarisha usimamizi wa matumizi salama ya mionzi nchini kwa kufanya ziara maalum katika Kanda ya Ziwa. Ziara hiyo, iliyohusisha Bodi na Menejimenti ya TAEC, ililenga kukagua na kujionea utendaji kazi wa ofisi zake zilizopo Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Bandari ya Mwanza, Ofisi ya TAEC Nyegezi pamoja na Ofisi ya TAEC Sirari.

Katika hatua ya kwanza, wajumbe wa Bodi na Menejimenti walitembelea Uwanja wa Ndege wa Mwanza na kufanya mazungumzo na Meneja wa Uwanja wa Ndege Kanda ya Ziwa, Bi. Rose Comino. Alieleza namna TAEC inavyoshirikiana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege katika ukaguzi wa mashine za kukagulia mizigo (Baggage Scanners) na kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mashine hizo. Bi. Comino alibainisha kuwa mashine zote zinazotumika kwa ukaguzi wa mizigo zimekidhi matakwa ya kisheria kwa kupata vibali kutoka TAEC. Aidha, alieleza kuwa ujenzi mkubwa unaoendelea kiwanjani utakapokamilika, mashine za ziada za ukaguzi wa mizigo zitafungwa ili kuboresha zaidi huduma kwa abiria.

Mwenyekiti wa Bodi ya TAEC, Profesa Joseph Msambishaka, alisisitiza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano na kuboresha utekelezaji wa majukumu ya pamoja. Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Najat Kassim Mohammed, alitoa shukrani kwa mapokezi mazuri na kusisitiza kuwa ushirikiano mzuri uliopo ni chachu ya mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya kisheria ya TAEC.

Afisa Ukaguzi wa Mionzi wa TAEC, Bw. Stephani Kapama, alieleza kuwa ofisi hiyo hukusanya wastani wa sampuli 30 kila mwezi kutoka shehena za mizigo na kuzifanyia vipimo ili kubaini uwepo wa mionzi. Pia hufanya ukaguzi wa mionzi kila siku katika maeneo yenye shughuli nyingi za binadamu: eneo la kuhifadhia mizigo, eneo la abiria wanaowasili na eneo la abiria wanaoondoka. Aliongeza kuwa muda wa kuchakata vibali vya mionzi umepungua kutoka siku saba hadi siku moja pekee, hatua iliyoongeza ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa na huduma.

Bodi na Menejimenti waliendelea na ziara kwa kuonana na Meneja wa Bandari Kanda ya Ziwa, Bi. Rosemary Ndesamburo. Alieleza namna bandari inavyoshirikiana na TAEC hususani katika ukaguzi wa mashine za midaki zinazotumika kukagua mizigo. TAEC hukagua mashine hizo na kutoa vibali vya matumizi yake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za matumizi salama ya mionzi. Mamlaka ya Bandari Kanda ya Ziwa inasimamia jumla ya bandari saba ambazo ni Mwanza South, Mwanza North, Nansio (Ukerewe), Kemondo Bay, Bukoba, Musoma na Kisorya.

Bandari hizi ni kiungo muhimu cha usafirishaji wa abiria na mizigo ndani ya Ziwa Victoria na zinashirikiana kwa karibu na TAEC kuhakikisha usalama wa matumizi ya teknolojia ya mionzi.

Bodi na Menejimenti walitembelea pia ofisi ya TAEC iliyopo Nyegezi na kujionea utekelezaji wa kazi mbalimbali zinazotolewa na ofisi ya kanda katika kuhudumia wananchi wa Kanda ya Ziwa. Msimamizi wa Ofisi ya Kanda, Dkt. Suleiman Ameir Suleiman, alieleza kuwa ofisi hiyo hufanya kazi za kila siku ikiwemo utoaji wa elimu kwa shule na jamii juu ya matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia, ukaguzi wa vituo vinavyomiliki vyanzo vya mionzi, upimaji wa mionzi kwenye bidhaa za vyakula vinavyoingia na kutoka ndani ya kanda, upimaji wa viasili vya mionzi kwenye mazingira pamoja na utafutaji wa vyanzo vya mionzi vilivyopotea.

Ziara ya Bodi na Menejimenti ya TAEC katika Kanda ya Ziwa ilihitimishwa kwa kutembelea mpaka wa Sirari, ambapo wajumbe walikutana na viongozi kutoka taasisi mbalimbali za serikali zinazoshirikiana katika kutoa huduma kwa ufanisi mpakani hapo. Afisa Mkuu wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Godfrey Leonard, aliyemuwakilisha Meneja Msaidizi wa TRA Sirari, alieleza namna taasisi zote zilizopo mpakani zinavyoshirikiana kwa karibu kuhakikisha huduma zinatolewa kwa haraka na kwa ufanisi.

Taasisi zinazoshirikiana Sirari ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jeshi la Polisi Tanzania, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF), Ofisi ya Rais, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Wakala wa Vipimo, Wizara ya Madini, Jeshi la Wanyamapori, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu (SUMATRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Idara ya Uhamiaji Tanzania na Tanzania Bureau of Standards (TBS).

Mwenyekiti wa Bodi ya TAEC, Profesa Joseph Msambishaka, alieleza kuwa ziara hiyo ililenga kufika mpaka wa Sirari ili wajumbe wapya wa Bodi waweze kufahamu kwa undani namna TAEC inavyotekeleza majukumu yake katika eneo hilo. Alisisitiza kuwa ni busara Bodi kujionea kwa macho yake jinsi kazi za ukaguzi wa mionzi zinavyofanyika mpakani, hususan katika shehena za mizigo, ili kubaini uwepo wa uchafuzi wa mionzi au kuzuia usafirishaji holela wa vyanzo vya mionzi.

Bodi ilipata maelezo kutoka kwa Mkaguzi wa Mionzi wa TAEC, Bw. Kasoga, ambaye alieleza namna ofisi ya TAEC mpakani hapo inavyotekeleza majukumu yake ya kila siku katika kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za matumizi salama ya mionzi. Aidha, wajumbe walitembelea maabara ya TAEC Sirari na kupata maelezo juu ya namna inavyotumika katika ukaguzi wa sampuli za bidhaa mbalimbali, na kujionea vifaa na teknolojia zinazotumika kupima viwango vya mionzi.

Ziara hii imekuwa chachu ya mafanikio kwa wajumbe wa Bodi ya TAEC kujionea kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya Tume katika maeneo nyeti ya mipaka, viwanja vya ndege na bandari. Hatua hii imeimarisha ushirikiano wa taasisi za serikali katika kuhakikisha usalama wa wananchi dhidi ya mionzi na kuendeleza matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini. Mafanikio haya ni kielelezo cha dira ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kusimamia kwa maono makubwa na uongozi thabiti juhudi za kulinda afya na usalama wa Watanzania. Kupitia msisitizo wake wa kuimarisha taasisi za kitaifa na kuhimiza matumizi ya sayansi na teknolojia kwa maendeleo endelevu, taifa linaendelea kujengeka katika misingi imara ya usalama, uchumi na ustawi wa wananchi.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »