
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Mtumba Mhe. Anthony Mavunde , amevitaka vikundi vilivyonufaika na mkopo wa shilingi bilioni mbili uliotolewa kwa wajasiriamali wa jimbo hilo, kutumia fedha hizo kama zilivyokusudiwa ili kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo hiyo jijini Dodoma, Mhe.Mavunde amesema kuwa azma ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata nyenzo na mitaji ya kuwawezesha kupanua na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Amesema kuwa Mkopo huo umefadhiliwa na CRDB Bank kupitia CRDB Bank Foundation katika programu ya imbeju inayolenga kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati.
"Tumieni vizuri mikopo hiyo kwa kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za ujasiriamali ili iweze kuleta tija, kuwaimarisha kiuchumi na hatimaye kurejeshwa kwa manufaa ya wengine."amesema Mhe.Mavunde
Mhe.Mavunde amesema kuwa mikopo hiyo ni kama mbegu inayohitaji kutunzwa na kuendelezwa ili izae matunda yenye manufaa kwa mkopaji na jamii kwa ujumla.
“Mikopo hii ni mbegu. mkizitumia vizuri zitazaa matunda na kuwainua kiuchumi, lakini pia zitawawezesha wengine kupata fursa kama hii baada ya ninyi kurejesha kwa wakati,” amesisitiza
Aidha ameongeza kuwa dhamira yake ni kuona wananchi wa mtumba wanaachana kabisa na mikopo umiza maarufu kama ‘mikopo ya kausha damu’ na badala yake wanatumia fursa rasmi za kifedha zenye masharti nafuu na rafiki kwa maendeleo yao.
“Wananchi wa mtumba wakae mkao wa kula. kuna mipango mingi ya kuwawezesha kiuchumi inaendelea kuja, na lengo letu ni kuhakikisha kila mmoja anapata fursa ya kujikwamua,” ameongeza
Hata hivyo amewataka wanufaika kuchangamkia fursa hizo kila zinapojitokeza na kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili wengine nao wapate kunufaika na mpango huo.
kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa CRDB Bank Foundation,Bi. Tully Esther Mwambapa, amesema kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na serikali kupitia programu mbalimbali zinazolenga kuyawezesha makundi tofauti ya wananchi kiuchumi.
Amesema kuwa lengo la programu ya imbeju ni kuwajengea uwezo wajasiriamali kwa kuwapatia mitaji pamoja na elimu ya usimamizi wa biashara ili waweze kuendesha miradi yao kwa tija na ufanisi.
" Hadi sasa taasisi hiyo imetoa mikopo ya mitaji wezeshi yenye thamani ya shilingi bilioni 22.1, huku zaidi ya wajasiriamali milioni moja wakinufaika nchini kote."amesema
Amesema kuwa mikopo hiyo imekuwa chachu ya kuboresha ustawi wa kiuchumi wa jamii na kuchangia katika ukuaji wa pato la taifa kupitia shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa na wanufaika.
Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru CRDB kwa kuwagusa moja kwa moja katika maisha yao na kuahidi kuitumia mikopo hiyo katika shughuli za uzalishaji mali pamoja na kuirejesha kwa wakati ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi katika maeneo mbalimbali nchini.
hafla hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kuimarisha uchumi wa wananchi wa mtumba na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya taifa.

EmoticonEmoticon