
Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais (Uwekezaji) Dkt. Fred Msemwa ametoa wito kwa vijana hususani walioko vyuo vikuu kujenga utamaduni wa kujifunza kuhusu uwekezaji, kwa kuwa wana faida ya kuwa na uwezo wa kiutendaji na utimamu wa kimwili.
Dkt. Msemwa, ametoa wito huo leo katika hafla ya uzinduzi wa Klabu ya Uwekezaji kwa Vijana (YIC) katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dar es Salaam, ambapo amesisitiza kuwa Dira 2050 imewapatia vijana umuhimu mkubwa kwa kuwaona wao kama rasilimaliwatu Muhimu.
“Dira inawatambua nyinyi kama rasilimali muhimu ya Taifa, inasisitiza kuwaandaa kuwa na ujuzi wa hali ya juu ili muiwezasha nchi kushindana kimataifa.” Alisema Dkt. Msemwa.
Katika mazungumzo yake na vijana hao, aliwapa changamoto ya kujiwekea msingi imara wa kiuchumi, akawafundisha nguzo nne muhimu zilizohusisha; kuwa na malengo, kujenga mtizamo sahihi, kujifunza kuweka akiba na kuwekeza, na kujifunza tabia ya kufanya zaidi.
Vile vile, Katibu Mkuu amewakumbusha kuwa Elimu ya Fedha, Ujasiriamali, Uwekezaji kwenye mifuko ya kijamii, na ujuzi wa Kuanzisha na Kusimamia Biashara, iliyokuwa ikitolewa katika hafla hiyo ilikuwa muhimu kwa kuwa inajibu changamoto zao binafsi na za jamii.
Ufunguzi wa Klabu hiyo, ni sehemu ya utekelezaji wa program ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) unaolenga kukuza elimu ya fedha, ujasiriamali na utamaduni wa uwekezaji miongoni mwa vijana na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini.










EmoticonEmoticon