Samson Abeid akitoa neno la shukrani wakati wa hafla ya kuwaaga wanafunzi wa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) waliopata ufadhili wa kwenda kusomea taaluma ya madini.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. William Anangisye akimkabidhi Samson Abeid nyaraka za udhamini katika hafla hiyoSamson Abeid akipongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baada ya kupokea nyaraka za ufadhili kutoka kwa Meneja wa Barrick nchini, Dk. Melkiory Ngido (kushoto)
Samson Abeid na Wanafunzi wenzake waliopata ufadhili wakiwa na bendera ya kampuni ya Barrick
Wanafunzi waliopata ufadhili wa Barrick kusomea taaluma ya Madini nchini Afrika ya Kusini katika picha ya pamoja na viongozi wa UDSM na Barrick nchini.
****
"Nilipopata taarifa kuwa nimekuwa miongoni mwa washindi wa ufadhili (Scholarship) ya kampuni ya Barrick ya kusomea kozi ya Uhandisi wa Madini na Uchakataji wa Madini (Metallurgy and Mineral Processing Engineering} katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini nilijisikia kama nipo ndotoni, japokuwa salamu za kunipongeza ziliendelea kumiminika kwangu kutoka kwa wanafunzi wenzangu wa mwaka wa kwanza niliokuwa nasoma nao katika Shule ya Madini na Sayansi ya Miamba (SoMG) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam", amesema kwa furaha Samson Rashid Abeid, mmoja wa washindi watano wa nafasi za ufadhili wa Barrick nchini kusomea taaluma ya madini.
Katika mahojiano hivi karibuni, Samson anasema kuwa fursa hii kwake anaiona kama muujiza kwa kuwa amezaliwa kwenye sehemu yenye shughuli za madini katika kitongoji cha Bugarama kilichopo jirani na mgodi wa dhahabu wa Barrick Bulyanhulu wilayani Msalala na ndoto yake kubwa tangu utotoni ilikuwa ni kusomea utaalamu wa madini , safari aliyoianza na kusoma kwa bidii na kujikuta baada ya elimu ya sekondari anachaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea fani hiyo, sasa imekuwa bahati amepata nafasi ya kusomea fani hiyo aipendayo katika Chuo Kikuu cha nje ya nchi.
“Kitu kingine ambacho naona kama muujiza ni kwamba katika shule ya msingi niliyosoma ya Bugarama miundombinu yake na mazingira yake mazuri ya kusomea yamejengwa na mgodi wa Barrick Bulyanhulu na baada ya kupita muda mrefu sasa imetokea katika ushindani mkubwa nimekuwa miongoni mwa wanafunzi walioshinda nafasi za ufadhili wa kampuni ya Barrick.ambayo imeniwezesha kuelekea katika safari ya kutimiza ndoto yangu kuanzia shule ya msingi na sasa Chuo kikuu”, amesema Samson Abeid.
Akielezea historia yake fupi ya elimu alisema elimu ya msingi katika Shule ya Bugarama na alipomaliza alichaguliwa kujiunga na Sekondari ya ufundi ya Moshi Tech ambayo imemjenga zaidi katika safari ya kutimiza ndoto yake akaweza kupata vigezo vya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea kozi aliyoipenda inayohusiana na utaalamu katika sekta ya madini.
Uwekezaji katika kizazi kijacho cha wataalamu wa sekta ya madini
Samson anasema wakati serikali ya Tanzania inakwenda kasi katika kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini,kunahitajiwa uwekezaji wenye mipango mikubwa utakaowezesha miradi mbalimbali ya kimkakati inayoendelea kuanzishwa kuwa endelevu na sio tu kuwekeza kwenye fedha na teknolojia bali kuwekeza pia katika kupata wataalamu wa kuendesha miradi kwa kipindi cha sasa na miaka ya mbele.
Ameendelea kueleza kuwa kuwa bila kufanya uwekezaji wenye mtazamo wa kujenga biashara endelevu kwa miaka mingi, kuna hatari ya biashara nyingi hususani katika sekta nyeti kama za madini na mafuta kuendelea kutegemea wataalamu wa kigeni na watanzania kuachwa nyuma na kubaki kama watazamaji.
Anashauri kuwa kuna haja ya kuwapatia vijana wengi wa kitanzania fursa za kusoma fani zenye wataalamu wachache katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi sambamba na kuanzishwa Progamu mbalimbali za kuwanoa vijana wa kitanzania wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya ufundi kwa kuwapatia mafunzo ya vitendo kwa ajili ya kuwaanda kwendana na mabadiliko yanayotokea katika kila sekta na kushika nafasi za uongozi katika miaka ya mbele.
Akiongea kuhusu kupata nafasi ya Ufadhili wa Barrick kusomea taaluma ya madini nchini Afrika ya Kusini Samson, anaeleza kuwa anajivunia kuwa miongoni mwa wanafunzi wachache waliochaguliwa kwa kuwa ushindani wa kuipata nafasi ulikuwa mkubwa sambamba na mchujo mkali uliofanywa na wataalamu mbalimbali ili kuhakikisha na kujiridhisha kuwa wanachukua watu wenye uwezo, makini na waliopo tayari kujifunza."Nina uhakika tutafanya vizuri hatutamuangusha mdhamini wetu na taifa letu kwa ujumla",amesisitiza.
Anasema moja ya ndoto kubwa aliyokuwa nayo katika maisha yake ni kufanya kazi katika kampuni kubwa na yenye mifumo mizuri ya kazi, jambo ambalo linaelekea kutimia kutokana na kampuni ya Barrick kutangaza pia fursa kuwapatia ajira pindi watakapomaliza elimu sambamba na kuwapatia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa vitendo wakati wote watakapokuwa masomoni.
Kuhusu mambo yanayomvutia kutamani kufanya kazi katika kampuni ya Barrick alisema ni mengi mbali na kupata maslahi mazuri na utaalamu wa viwango vya kimataifa pia anavutiwa na jinsi inavyotekeleza sera zenye mtazamo wa kujenga jamii endelevu zinazoenda sambamba na utekelezaji wa malengo endelevu ya milenia ya umoja wa mataifa.
"Inafurahisha kuona kampuni inayapa kipaumbele masuala ya msingi katika kujenga biashara endelevu kama vile utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji,usalama wa wafanyakazi wake ,kushirikiana na jamii zilizopo katika maeneo inakofanyia biashara zake kama ambavyo inafanya kazi na wazabuni wa ndani kuhakikisha inafanya manunuzi ya ndani ya nchini kwa asilimia kubwa ,kuendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa wazabuni ili nao biashara zao zikuwe na kuwa endelevu bila kusahau kufanikisha miradi mbalimbali ya kusaidia jamii hususani katika sekta za elimu,afya,maji salama na uboreshaji wa miundombinu ya barabara", amesema Samson.
Samson, anaeleza kuwa anaamini kuwa hadi kufikia kuhitimu shahada yake ya kwanza nchini Afrika ya Kusini, atakuwa amejifunza mambo mengi yatakayomsaidia katika safari yake ndefu ya kuwa mtaalamu wa madini sambamba na kuwa mbunifu na kutoa mawazo ya kitaalamu yanayowezesha kukabili changamoto na kuwezesha sekta ya madini nchini Tanzania kusonga mbele kwa mafanikio makubwa.
Amemalizia kwa kutoa ushauri kwa wawekezaji wengine wanaotoka nje na ndani ya nchi kuiga mfano wa Barrick kwa kuwa na mtazamo wa kujenga biashara endelevu sambamba na kuwa na programu za kuandaa wataalamu wazawa kwa kuwawezesha kupata elimu na utaalamu kama ambavyo imedhamini wanafunzi watano kusomea utaalamu wa fani ya madini nje ya nchi.
"Programu kama hii ni muhimu kwa kuwanoa vijana wasomi kupata ujuzi wa viwango vya kimataifa ,natamani kuona pia idadi ya vijana wanaochukuliwa katika Programu hii kuongezwa zaidi ya sasa ili inufaishe vijana wengi wa kitanzania", amesisitiza.




EmoticonEmoticon