Na Mwandishi Wetu
Wizara ya Nishati imetoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Monduli kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake watumie nishati safi ya kupikia, ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay kwenye ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa maagizo ya Ofisi ya Makamu wa Rais yanayohimiza matumizi ya nishati safi katika taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100, Wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha.
Mlay amesema umefika wakati kwa wananchi kubadili mtazamo na kuachana na jitihada za kutafuta kuni au magunia ya mkaa, na badala yake kuelekeza nguvu katika matumizi ya nishati safi ambayo ni salama kwa afya na mazingira.
“Mazingira ni ajenda ya dunia nzima, na Rais wetu ni kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Hivyo ni wajibu wetu kuunga mkono dhamira yake kwa kukaa pamoja, kujadiliana na kubuni mikakati ya kuwatoa wananchi kwenye matumizi ya nishati zisizo salama na kuwapeleka kwenye matumizi ya nishati safi,” amesisitiza.
Aidha, Mlay amewapongeza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutekeleza maagizo ya Serikali kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi mbalimbali.
Amesema si rahisi kwa Serikali kufahamu changamoto zilizopo katika kila eneo, hivyo mchango wa viongozi wa halmashauri ni muhimu kwani wanajitoa kwa dhati kufichua changamoto zilizopo bila hata kulipwa.

“Serikali inatambua jitihada hizi na inathamini sana taarifa za changamoto zinazowasilishwa, jambo linalowezesha kuchukuliwa kwa hatua stahiki kwa manufaa ya wananchi,” ameongeza.










EmoticonEmoticon