Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga, ametembelea Kata za Mkako na Kihangimahuka katika mwendelezo wa ziara yake ya kuwashukuru wananchi kwa ushindi mkubwa waliompatia yeye na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lihale, Mhe. Kapinga aliahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Wilaya pamoja na taasisi husika ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hususan katika sekta za miundombinu, maji na umeme.
“Serikali ipo pamoja nanyi, na mimi kama Mbunge wenu nitaendelea kushirikiana na viongozi wa wilaya na taasisi zote kuhakikisha changamoto zenu zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu".
Katika kuonesha dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo ya elimu, Mhe. Kapinga alitoa msaada wa bati 50 za geji 28 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.7 pamoja na kiasi cha shilingi laki tano kwa ajili ya ununuzi wa kenchi, kwa ajili ya ujenzi wa chumba kimoja cha darasa katika Shule ya Msingi Liale.
Aidha, alitembelea Shule ya Sekondari Kihangimahuka ambapo alikabidhi kompyuta moja yenye thamani ya shilingi milioni 2.5 pamoja na mifuko 50 ya saruji yenye thamani ya shilingi laki tisa, ikiwa ni jitihada za kuimarisha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji. Vilevile, aliahidi kuipatia shule hiyo mashine ya fotokopi kabla ya kumalizika kwa mwezi Februari 2026.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Vijijini alisema Serikali itaendelea kuleta miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jimbo la Mbinga Vijijini, hususan katika sekta ya afya, alieleza kuwa jumla ya wahudumu wa afya 100 wameanza kuwasili katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri, wakiwemo madaktari zaidi ya 10, manesi wenye shahada zaidi ya 30 pamoja na wataalamu wengine wa afya.
Aidha, alimpongeza Mhe. Kapinga kwa mchango wake katika kuboresha huduma za afya, ikiwemo kuwasaidia kupata gari la wagonjwa (ambulance) ambalo limekuwa likisaidia kwa kiasi kikubwa kusafirisha wagonjwa, pamoja na ahadi yake ya kukarabati jengo la kinamama katika Zahanati ya Lihale.
Kwa upande wa wananchi wa Kata za Mkako na Kihangimahuka walimpongeza na kumshukuru Mbunge wao kwa kuendelea kutoa michango yake binafsi katika miradi ya maendeleo, wakieleza kuwa hatua hizo zimeongeza mshikamano na ari ya wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Mbunge huyo wa kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi, viongozi na taasisi za serikali kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu katika Jimbo la Mbinga Vijijini.
EmoticonEmoticon