Mkuu wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Januari 20,2026 Makao Makuu ya JKT Chamwino Mkoani Dodoma kwa niaba ya MKUU wa JKT.
Mkuu wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena,akisisitiza jambo kwa Waandishi wa Habari leo Januari 20,2026 Makao Makuu ya JKT Chamwino Mkoani Dodoma kwa niaba ya MKUU wa JKT .
Na.Alex Sonna-DODOMA
JESHI la Kujenga Taifa JKT limetangaza nafasi za kujitolea kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mwaka 2026, vijana wote kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wenye sifa za kujiunga na Jeshi hilo huku watakaopata nafasi hizo wametakiwa kuripoti katika kambi za JKT kuanzia February 27 hadi Machi 4, mwaka huu.
Akizungumza leo Januari 20,2026 na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya JKT Chamwino Mkoani Dodoma kwa niaba ya MKUU wa JKT,Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema usaili utaanza Januari 26, mwaka huu kupitia Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar.
Amesema utaratibu wa vijana kuomba mafunzo hayo unaratibiwa chini ya ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya na vijana wenye elimu ya kuanzia darasa la saba hadi chuo kikuu wanazo sifa za kuomba, akisema watakaochaguliwa wataanza kujiunga katika kambi mbalimbali za JKT kuanzia February 27 hadi Machi nne mwaka huu.
"Mafunzo haya ni bure wazazi au walezi wasikubali kurubuniwa kutoa fedha ili vijana wao wapate nafasi za kujiunga na mafunzo hayo," amesema Brigedia Jenerali Mabena.
Brigedia Jenerali Mabena, amesema Jeshi hilo limeweka mkazo maalumu kwa vijana wenye ujuzi wa masomo ya kompyuta kuanzia ngazi ya Stashahada hadi Shahada ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani.
“Kipaumbele kitakuwa kwa vijana wenye taaluma za Stashahada ya Teknolojia ya Habari, Stashahada ya Mifumo ya Taarifa za Biashara, Stashahada ya Sayansi ya Kompyuta, Stashahada ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Stashahada ya Usalama Mtandaoni na Forensics ya Kidigitali,” amesema Brigedia Jenerali Mabena.
Aidha, ametoa wito kwa vijana wenye sifa kujitokeza katika maeneo yao ya vijiji, kata na tarafa kujiandikisha, akisisitiza kuwa nafasi hizo haziuziwi na kwamba kumekuwa na matapeli wanaojaribu kutumia mwanya huo kuwaibia wananchi.
“Nafasi hizi hazihitaji malipo yoyote. JKT Makao Makuu haina jukumu la kuandikisha, kila kitu kimepelekwa kwenye halmashauri, wilaya na mikoa. Wananchi wajihadhari na utapeli,” amesisitiza
Amesema kutokana na matumizi makubwa ya mitandao ya kidigitali nchini, JKT imeendelea kuwaandaa vijana kuielewa na kuitumia kwa maendeleo, ikiwemo kuongeza kipato kupitia ubunifu na fursa za kidigitali.
Brigedia Jenerali Mabena ameongeza kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa amewakaribisha vijana wote wa Tanzania Bara na Visiwani kujiunga na mafunzo hayo ya kujitolea kwa mwaka 2026.
Aidha amesema sifa za mwombaji awe raia wa Tanzania.Kwa Vijana wenye elimu ya darasa la saba kutoka Tanzania Bara na Vijana wenye elimu ya kidato cha Pili kutoka Zanzibar.
Amesema umri ni kuanzia miaka 16 hadi 18, waliomaliza kuanzia Mwaka 2022,2023, 2024, 2025 na awe na cheti halisi cha kumaliza elimu ya msingi na Kidato cha Pili. Vijana wenye elimu ya kidato cha nne umri usiwe zaidi ya miaka 20, waliomaliza Elimu ya Sekondari kuanzia Mwaka 2022,2023, 2024, 2025 na awe na cheti halisi cha kumaliza elimu ya sekondari na cheti halisi cha matokeo
Pia awe na ufaulu wa daraja la Kwanza hadi daraja la nne. Kijana mwenye daraja la nne awe na ufaulu waalama kuanzia 26 hadi 32.
Amesema kuwa vijana wenye elimu ya Kidato cha Sita umri usiwe zaidi ya miaka 22,waliomaliza elimu ya Sekondari kuanzia mwaka 2022, 2023,2024, 2025 na awe na cheti halisi cha kumaliza Elimu ya Sekondari na cheti halisi cha matokeo
Pia awe na ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi daraja la Nne. Vijana wenye elimu ya Stashahada umri usiwe zaidi ya miaka 25,awe na vyeti vya Sekondari na cheti cha Chuo. Vijana wenye Elimu ya Shahada umri usiwe zaidi ya miaka 26,awe na vyeti vya Sekondari na cheti cha Chuo
Aidha vijana wenye elimu ya Shahada ya Uzamili umri usiwe zaidi ya miaka 27, awe na vyeti vya Sekondari na cheti cha Chuo. Awe na afya njema, akili timamu na asiwe na alama yoyoteya michoro mwilini (Tattoo).

EmoticonEmoticon