BILIONI 151 RUWASA MWANZA KUNG’ARISHA HUDUMA YA MAJI VIJIJINI

January 29, 2026


Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Mwanza unaendelea na utekelezaji wa miradi 71 inayoendelea kujengwa katika wilaya mbalimbali ambapo ikikamilika inatarajiwa kupandisha wastani wa huduma ya maji vijijini mkoani humo kutoka wastani wa asilimia 73 ya sasa hadi kufikia asilimia 88 hivyo kuendelea kuimarisha uchumi wa mtu mmoja na jamii kwa ujumla.

Miradi hiyo inatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 151 kutoka vyanzo mbalimbali vya fedha ikiwemo Serikali Kuu, Programu ya lipa kwa matokeo (PforR) na Mfuko wa Taifa wa Maji.

Hayo yameelezwa na Meneja wa RUWASA mkoa wa Mwanza Mha. Godfrey Sanga wakati wa ziara ya timu ya Menejimenti ya taasisi hiyo kutoka Makao Makuu inayofanya tathimini ya uendeshaji wa huduma ya maji vijijini inayotolewa na Vyombo vya Utoaji Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) kote nchini.

Mha. Sanga alisema miradi hiyo ipo katika hatua tofauti za ujenzi ikiwemo mradi wa maji wa Ukiriguru wenye vijiji 19, na Ilujamahate-Buhingo utakaohudumia vijiji 16, na kwamba itakapokamilika itainua huduma kufikia vijiji vingi zaidi mkoani humo na kuendelea kukamilisha dhamira ya serikali ya kumtua mama wa kijijini ndoo kichwani.
Katika siku ya kwanza mkoani Mwanza, timu ya Menejimenti ya ukaguzi na tathimini ya kazi za CBWSO ilitembelea Chombo cha Nyamwaki kilichopo wilayani Magu na Miswaso kilichopo wilaya ya Kwimba ambapo zoezi hilo litaendelea katika wilaya za Misungwi na Segerema.





Share this

Related Posts

Previous
Next Post »