Yajipanga kusambaza kwa nchi jirani
Rukwa
Kampuni ya Upendo Group Limited, inayojihusisha na uchimbaji wa makaa ya mawe katika eneo la Muze, Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, imeeleza kuwa inatarajia kuanza uzalishaji rasmi mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu ambapo inapanga kuzalisha tani 10,000 kwa mwezi na kusambaza bidhaa katika soko la ndani na mataifa ya jirani.
Akizungumza wakati wa ziara ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Joseph Kumburu, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Cassiano Kaegele, amesema makaa ya mawe hayo yanatarajiwa kuuzwa katika nchi za Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya na Zambia, kutokana na ukaribu wa mgodi na mipaka ya mataifa hayo.
Kaegele amesema hatua hiyo itapunguza gharama kwa wanunuzi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitegemea makaa ya mawe kutoka mikoa ya mbali kama Ruvuma na Njombe.
Ameongeza kuwa uzalishaji huo pia utachochea shughuli za kiuchumi kwa mkoa wa Rukwa na maeneo ya jirani.
Katika uchimbaji wa eneo hilo lenye leseni 33 za uchimbaji mdogo wa madini, kampuni imeajiri wafanyakazi 34 wa kudumu na inaendelea kushirikiana na jamii kwa kuboresha miundombinu ikiwemo shule na barabara.
Aidha, soko la ndani linatarajiwa kukua zaidi hususan katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Kigoma.
Kaegele amesema mwitikio wa vijana kujiingiza katika shughuli za uchimbaji umekuwa mkubwa, hasa kwa kazi zisizohitaji utaalam wa juu, hatua inayosaidia kuongeza ajira na kipato katika jamii.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Kumburu, ameendelea kutoa elimu na uhamasishaji kuhusu uwekezaji katika sekta ya madini, huku akisisitiza ushirikiano kati ya Serikali na wawekezaji ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi.







EmoticonEmoticon