Timu ya mpira wa miguu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeilaza timu ya WCF kwa jumla ya magoli matano kwa sifuri.
Mchezo huo uliochezwa Novemba 27, 2025, katika uwanja wa Highland mkoani Morogoro, ulianza kwa kasi kubwa ambapo dakika ya 15 Fortinatus Patrick alifungua ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penati, na kufanya “mazingira ya uwanja” kuanza kuwa safi.
Bao hilo lilidumu hadi dakika ya 33 ambapo mfungaji huyo huyo, Fortinatus Patrick, alipachika bao la pili lililoipeleka NEMC mapumzikoni wakiwa kifua mbele, huku “mazingira” yakiendelea kupendeza uwanjani.
Kipindi cha pili kilipoanza dakika ya 46, Fortinatus Patrick aliendeleza ubabe kwa kufunga bao la tatu, kabla ya kiungo Ismail Jemba kuongeza la nne dakika ya 51.
Kama ilivyo desturi ya NEMC kutoridhishwa na uchafuzi wa mazingira nchini na kuendelea kuhimiza usafi kote nchini, vivyo hivyo hawakuridhika na matokeo hayo ya 4–0. Dakika ya 62, Emmanuel Mlungwana alipiga shuti kali kutoka katikati ya uwanja lililopenya kati ya miguu ya golikipa wa WCF na kutinga wavuni, likiwa bao la tano kwa NEMC.
NEMC ipo mkoani Morogoro kushiriki michezo ya SHIMMUTA 2025 kama sehemu ya kuimarisha afya za watumishi wake pamoja na kuendelea kutoa hamasa kuhusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini. Kwa mwaka huu, timu za NEMC zimefadhiliwa jezi na vifaa vya michezo kupitia miradi yake miwili — Adaptation Fund na EHPMP — huku zikitumia jezi hizo kueneza jumbe mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabianchi na udhibiti wa matumizi ya zebaki (mercury).












EmoticonEmoticon