
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Regina Qwaray akizungumza na Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi wakati akifungua kikao kazi kilicholenga kutambua changamoto za Utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake kilichofanyika leo Novemba 27,2025 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa kwa niaba ya Waziri wa Ofisi hiyo.

Sehemu ya washiriki wakisiliza hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Regina Qwaray (hayupo pichani) wakati akizungumza na Maafisa Sheria na Maafisa Utumishi wakati akifungua kikao kazi kilicholenga kutambua changamoto za Utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake kilichofanyika leo Novemba 27,2025 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa kwa niaba ya Waziri wa Ofisi hiyo.
...
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Regina Qwaray, amewataka Maafisa Utumishi na Maafisa Sheria kote nchini kuzingatia kikamilifu Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 na kanuni zake huku akionya uzembe na ukiukwaji wa taratibu za kiutumishi umeendelea kuitia serikali hasara kubwa isiyo ya lazima.
Mhe.Qwaray ameyasema hayo leo Novemba 27,2025 Mkoani Iringa wakati akifungua kikao kazi chenye lengo la kutambua changamoto za utekelezaji wa Sheria ya utumishi wa umma sura 298 kwa niaba ya Waziri wa Ofisi hiyo.
Amewahimiza washiriki kuhakikisha usimamizi wa rasilimali watu unazingatia misingi ya Kazi na Utu kama inavyoelekezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
“Rasilimali watu ikisimamiwa vibaya, utendaji kazi hushuka, na pale utendaji unaposua sua hata uchumi nao hauwezi kukua. Hali hiyo pia huleta malalamiko na kuondoa imani ya wananchi kwa serikali yao, jambo ambalo ni hatari kwa ustawi na usalama wa Taifa,” amesema Mhe.Qwaray
Aidha amesema kuwa ofisi yake imekuwa ikipokea barua nyingi za kuomba ufafanuzi wa mambo ambayo tayari yanaelekezwa katika nyaraka rasmi, akibainisha kuwa hali hiyo ni dalili ya kutokuwajibika ipasavyo kwa wasimamizi wa rasilimali watu.
Mhe.Qwaray,ameeleza kuwa mashauri ya nidhamu yameendelea kuisababishia serikali hasara, kutokana na makosa madogo madogo ya kisheria yanayofanywa na baadhi ya maafisa, ikiwemo uandishi usio sahihi wa hati za mashtaka, uundaji wa kamati usiozingatia taratibu, kushindwa kuzingatia muda, na kutowapa watuhumiwa haki zao za msingi.
“Kutofuata sheria na kanuni wakati wa kushughulikia mashauri ya nidhamu kunaisababishia serikali hasara bila sababu. Nasisitiza, zingatieni kikamilifu taratibu zilizowekwa,” amesema
Hata hivyo amewataka washiriki kuwa wabunifu, kushirikiana na kujenga uongozi wenye thamani unaoenziwa na wanaowaongoza, huku wakitambua wajibu wa kuhakikisha haki za watumishi zinatolewa kwa wakati.
“Haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa. Mtumishi akipata haki yake kwa wakati anapata ari ya kufanya kazi. Hakikisheni mnasimamia hilo,” amesisitiza.
Pia amewataka watumishi kutanguliza maslahi ya Taifa na kuendelea kuwa mfano wa uzalendo, uadilifu na uvumilivu, akisema Watumishi wa Umma ni kioo cha Serikali na walinzi wa amani ya nchi.
Amewakumbusha umuhimu wa kila mtumishi kuwa na nyaraka muhimu mezani kwake, zikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na Mpango Mkakati wa taasisi husika.
Amesema kuwa anaamini mada zitakazotolewa katika kikao kazi hicho zitawawezesha washiriki kuimarisha uelewa wa sheria, kanuni na taratibu, na kwamba mafunzo hayo yataboresha utendaji na utoaji wa huduma kwa umma.
Aidha amewataka washiriki kuzingatia maadili, kupinga rushwa na kuwa viongozi wa mfano.
“Rushwa ni adui wa haki. Kiongozi asiyepinga rushwa hawezi kusimamia haki wala kulinda rasilimali za nchi,” amesema
EmoticonEmoticon