MARY CHATANDA ATIMIZA AHADI YA NG'OMBE WAWILI KWA MAGEREZA

March 11, 2026


Na: Mwandishi Wetu, KOROGWE

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (MCC) na Mbunge wa Viti Maalum wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Mary Chatanda, ametimiza ahadi yake ya kutoa ng'ombe wawili wa maziwa kwa Magereza mawili ya wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Hafla hiyo imefanyika Machi 09, 2026, ambapo viongozi wa CCM ngazi ya wilaya walimwakilisha Chatanda Katika kukabidhi ng'ombe hao. Katika Gereza la Kwamngumi viongozi wa Chama walikabidhi ng'ombe wa maziwa kwa kikundi cha wake wa Askari Magereza huku ng'ombe mwingine akikabidhiwa kwa uongozi wa Gereza la Manundu.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Korogwe, Thobias Nyakusagira alisema "Utoaji wa ng'ombe hawa ni utekelezaji wa ahadi ya Mama Mary Pius Chatanda baada ya kufanya ziara Magerezani na akapokea changamoto na leo tupo hapa kutekeleza ahadi yake." 

Kwa upande wa Katibu wa CCM wilaya Korogwe Mjini, Evarist Mluge alisema "Mama Chatanda wakati wa ziara yake ya kuimarisha Chama, alitembelea makundi maalum yakiwemo wanawake na wafungwa ambapo alipokea maombi ya ng'ombe wa maziwa na leo tuna furaha kuwa ahadi yake ameitekeleza kwa vitendo."


Katika hatua nyingine, viongozi wa kikundi cha wake wa Askari Magereza wamemshukuru Mama Chatanda kwa kuwaunga mkono katika jitihada zao za kujikomboa kiuchumi kwani ng'ombe huyo atawasaidia kuongeza kipato chao. Katika hatua nyingine, uongozi wa Gereza la Manundu wameahidi kumtunza ng'ombe huyo kwani atasaidia kupatikana maziwa yatakayosaidia kuimarisha afya za wafungwa.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wa UWT wilaya, Faida Bayagumu, Katibu wa UWT wilaya, Suzan Mandia na Diwani wa Kata ya Kilole ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Ally Mkwavingwa. Viongozi hao wamesisitiza kushirikiana na Magereza hayo katika kutatua changamoto zao kwani hayo ndiyo maelekezo ya Chama chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake Taifa, Dk. Samia Suluhu Hassan ya kutatua changamoto za wananchi kwa wakati ili kujenga ustawi wao.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »