📌 Unalenga kuongeza uelewa wa Watanzania juu Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia
📌 waambatana na Kauli mbiu isemayo Nishati safi ya kupikia okoa maisha na mazingira
📌Mwitikio wa wananchi maeneo ya vijijini waongezeka kwa kasi
Imeelezwa kuwa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia ni nyenzo muhimu ya kufanikisha malengo ya Taifa ya kuhakikisha wananchi wanapika kwa kutumia nishati safi, salama na rafiki wa mazingira.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 27, 2025 Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati Bi. Neema Chalila Mbuja,wakati akizungumza katika Kipindi cha Joto la Asubuhi kinachorishwa na Efm.
“Mkakati wa Mawasiliano wa nishati safi ya kupikia ni daraja muhimu linalounganisha wananchi, wadau wa maendeleo, na Serikali katika juhudi za kuongeza uelewa wa matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira kwani kupitia mkakati huu, taarifa sahihi na za wazi zinawafikika wananchi kwa urahisi ili kusaidia jamii kuelewa faida za kutumia nishati safi lakini pia Mawasiliano madhubuti ili kuchochea mabadiliko ya tabia kwa kuwapa watumiaji taarifa zinazohitajika nakufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya nishati”.Amehimiza Bi. Mbuja.
Aidha Bi. Mbuja ameendelea kusisitiza kuwa utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia unatekeleza pia makubaliano ya kimataifa yanayolenga kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa pamoja na kupunguza athari za kimazingira ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi watumie nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.
Ameongeza kuwa katika kutoa elimu ya nishati safi ya kupikia Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Nishati kinaenda na Kauli mbiu isemayo Nishati safi ya kupikia okoa maisha na mazingira,kwani kauli mbiu hii inalenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kulinda afya za wananchi, kupunguza gharama za maisha, na kuimarisha uchumi kwa kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma,elimu na miundombinu muhimu ya kutumia nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake Mhandisi Mwandamizi Utafiti Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bi. Catherine Mwegoha ameeleza kuwa Mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya kupikia ni dhana muhimu ya kufanikisha malengo ya Taifa ya kuhakikisha usalama, uendelevu na urahisi wa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia huku akieleza kuwa TANESCO imeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia lengo likiwa ni kuhakikisha usalama, uendelevu na urahisi wa upatikanaji wa nishati hizo Kuokoa muda jikoni, Kupunguza gharama za matumizi pamoja na kupunguza athari za kimazingira na afya kwa watumiaji.
Naye Mhandisi Miradi kutoka Wakala wa Nishati vijiijini(REA) Bi. Raya Majallah amethibitisha kuwa mwitikio wa wananchi juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa vijijini umeongezeka kwani wameendelea kutoa majiko kwa bei ya ruzuku. na kupitia ruzuku hiyo wananchi wameendelea kununua majiko kwa wingi hivyo jitihada hizo zinaonyesha hadi kufikia 2034 asilimia 80% ya wananchi watakua wamehamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.





EmoticonEmoticon