SERIKALI YATOA MWONGOZO KWA WAZAZI NA WALEZI KUHUSU USALAMA WA MTOTO MTANDAONI

November 27, 2025

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima,akizungumza wakati wa Mkutano na Watoto wa Shule ya Martin Luther jijini Dodoma.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima,akizungumza wakati wa Mkutano na Watoto wa Shule ya Martin Luther jijini Dodoma.

Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Makundi Maalum, Sebastian Kitiku,akizungumza wakati wa Mkutano na Watoto wa Shule ya Martin Luther jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima (hayupo pichani),akizungumza wakati wa Mkutano na Watoto wa Shule ya Martin Luther jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI imeitaka jamii kuongeza ulinzi kwa watoto katika kipindi cha likizo, kufuatia kuongezeka kwa matukio ya ukatili na hatari za kimtandao zinazowakumba watoto wanapotumia muda mrefu nyumbani bila uangalizi wa kutosha.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima,wakati akizungumza katika Mkutano na Watoto wa Shule ya Martin Luther jijini Dodoma ambapo amesema kuwa kasi ya maendeleo ya teknolojia imeongeza fursa kwa watoto, lakini pia imeleta changamoto kubwa zinazohitaji uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi na walezi.

Dkt. Gwajima amebainisha kuwa utafiti uliofanywa na Wizara kwa kushirikiana na UNICEF mwaka 2022 unaonyesha kuwa asilimia 67 ya watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 17 hutumia mitandao, huku wengine wakikumbana na ukatili wa kimtandao unaojumuisha kurubuniwa, vitisho na ulaghai.

“Maendeleo ya teknolojia ya habari hayakwepeki. Huu ni ulimwengu wa watoto wetu. Lakini bila uangalizi madhubuti, teknolojia hii inaweza kuwa chanzo cha madhara makubwa,” amesema Dkt.Gwajima

Kwa mujibu wa Waziri Gwajima , utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 4 ya watoto waliotumia mitandao wamewahi kufanyiwa ukatili wa kimtandao, huku asilimia 5 wakishawishiwa au kulazimishwa kutuma picha za utupu.

Aidha, ameongeza kuwa kipindi cha likizo kimekuwa hatari zaidi kwa sababu asilimia 60 ya ukatili kwa watoto hutokea majumbani, mara nyingi ukihusisha ndugu wa karibu.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuendesha Kampeni ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni, kuanzisha Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Usalama wa Mtoto Mtandaoni, na kufanya marekebisho ya sheria tatu muhimu Sheria ya Makosa ya Kimtandao, Sheria ya Mtoto na Sheria ya Msaada wa Kisheria.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema Wizara imeratibu uandaaji wa Mkakati wa Taifa wa Usalama wa Watoto Mtandaoni wa 2025/26–2029/30, ambao utaendelea kuimarisha ulinzi wa watoto na kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Ametoa wito  kwa wazazi, kuhakikisha watoto wanapewa mwongozo sahihi katika matumizi ya vifaa vya kielektroniki, kudhibiti muda wanaotumia kwenye runinga na simu, na kuzuia tabia ya watoto kulala na simu mikononi.

“Wazazi hakikisheni mnawafuatilia watoto wenu wanapotumia vifaa vya kielektroniki. Msiruhusu watoto kuangalia maudhui yasiyofaa wala kulala na simu. Hii ni hatari kwa usalama na afya yao,” amesisitiza.

Kwa upande wa watoto, Waziri ametoa tahadhari kadhaa, zikiwemo kuepuka kutembea peke yao maeneo hatarishi, kutozowea watu wasiowajua, kutojipiga au kutuma picha za faragha, na kuepuka kutoa taarifa binafsi mtandaoni.

“Kumbuka, ukishatuma kitu mtandaoni, unaweza kukifuta kwenye simu yako lakini huwezi kukiondoa kabisa mtandaoni,” aliwaonya watoto.

Hata hivyo ameishukuru Shule ya Martin Luther kwa kutoa fursa ya kukutana na watoto na jamii, huku akiwatakia likizo njema ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Makundi Maalum, Sebastian Kitiku amesema  tafiti zinaonyesha kuwa watoto wanapenda katuni hususani vipindi vya likizo lakini wanakutana na vitu visivyofaa mitandaoni hivyo lazima waelimishwe kuhusu matumizi mazuri.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »