📌 *Mkurugenzi Nishati Safi ya Kupikia apongeza jitihada za Shule zilizohamia kwenye nishati salama na rafiki kwa afya na Mazingira.*
📌 *Atoa wito kwa Wadau kuwekeza katika uzalishaji wa kuni/mkaa mbadala kutokana na kuhitajika kwake*
Mkurugenzi wa Nishati safi ya kupikia, Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay, ametoa wito kwa shule zote nchini kuhakikisha zinaachana na matumizi ya kuni na badala yake kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo gesi, majiko banifu, na mkaa mbadala.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya nishati safi ya kupikia inayotekelezwa chini ya mpango wa CookFund katika Mkoa wa Mwanza, Mlay amesema kuwa shule nyingi bado zinategemea kuni kama nishati ya dharura, hali inayochangia uharibifu wa mazingira na madhara kwa afya ya watumiaji.
“Katika ziara hii nimebaini Shule nyingi zinatumia kuni kama nishati ya dharura hivyo nitoe wito kwa uongozi wa shule mkishirikiana na Afisa Elimu kuanza kutumia mkaa mbadala ambao ni rafiki kwa mazingira na unachangia katika kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa." Amesema Mlay
Aidha, Bw. Mlay amepongeza baadhi ya shule ambazo tayari zimeanza kutumia nishati safi, ambazo hazifadhiliwi na mradi wa Cookfund ikiwemo shule ya Sekondari ya wavulana Musabe pamoja na Shule ya Msingi Buhongwa A akizitaja kuwa mfano bora kwa taasisi nyingine nchini.
Amesema matumizi ya nishati safi huchangia kwa kiasi kikubwa kulinda afya ya wanafunzi na walimu dhidi ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji, yanayosababishwa na moshi kutoka kwa kuni na mkaa wa kawaida.
“Tunapongeza juhudi za shule zinazohamia kwenye nishati safi ya kupikia kwani hii hatua ni kubwa katika kulinda afya, mazingira na hata kuongeza ufanisi wa shughuli za kila siku shuleni hivyo nitoe wito kwa shule zote ambazo bado hazijaanza kutumia nishati safi ya kupikia, kuanza kutumia nishati safi kwani ni nafuu na zinaokoa muda." Ameongeza Bw. Mlay
vilevile, Mlay amehimiza Serikali za Mitaa, Wakuu wa Shule na wadau wa elimu kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha taasisi za elimu zinapata vifaa vya kisasa vya kupikia kwa kutumia nishati safi.
Amesisitiza kuwa mradi wa CookFund na mipango mingine ya kitaifa iko tayari kusaidia shule zinazotaka kuhamia kwenye mfumo huo wa kisasa wa kupikia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024 - 2034 ambao unalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia.
Mlay ametoa wito kwa wawekezaji mbalimbali kujitokeza kuwekeza katika uzalishaji wa kuni na mkaa mbadala ili kufanikisha azma ya nchi kuhamia kwenye nishati safi na kulinda mazingira.
“Ni muhimu kuwekeza kwa dhati katika uzalishaji wa kuni na mkaa mbadala, hasa kwa ajili ya taasisi kwani kukosekana kwa wazalishaji hawa kunaweza kusababisha athari kubwa kiuchumi, kijamii na kimazingira hapo baadaye hivyo tunahimiza wadau wote kujitokeza, kushirikiana, na kuwekeza katika mabadiliko haya yenye tija kwa taifa na vizazi vijavyo”. Amesisitiza Bw. Mlay
Naye Afisa Elimu Taaluma Halmashauri ya Jiji la Mwanza Bw. Rodrick Kazinduki ameeleza kuwa kupitia mkakati wa Nishati Safi ya kupikia, Tanzania itaondokana na changamoto za uharibifu wa mazingira na afya zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi huku akieleza kuwa kupitia ushirikiano wa Serikali, Mashirika ya Kimataifa na jamii kwa ujumla, kuna matumaini kuwa shule nyingi zaidi zitaweza kuhama kutoka kwenye kuni na mkaa wa kawaida, na kuingia katika zama mpya za nishati safi, salama na endelevu.
EmoticonEmoticon