MASHINDANO YA NGALAWA YATUMIKA KUHAMASISHA USALAMA WA CHAKULA

October 13, 2025


Na Mwandishi Wetu, TANGA


MBIO za ngalawa baharini, zikijumuisha timu 12, zimekuwa kivutio katika Maadhimisho ya 44 ya Siku ya Chakula Kimataifa, ambapo hapa nchini, yanafanyika mkoani Tanga.


Mashindano hayo yaliyoratibiwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na wadau wengine, yamefanyika jana kwenye ufukwe wa Deep Sea jijini Tanga.

Kwenye shindano hilo lililofanyika kwenye umbali wa jumla ya kilomita 12 majini, nafasi ya kwanza ilichukuliwa na timu namba 010 iliyoongozwa na Idd Kileo na kusafiri kwa dakika 48:30.


Timu namba 012 iliyoongozwa na Amir Seleman ilichukua nafasi ya pili kwa kutumia dakika 48:49 wakati nafasi ya tatu ilichukuliwa na timu namba 009, ikiongozwa na Mahamud Rashid na ilitumia dakika 49:20.

Washindi hao watatunukiwa zawadi za ushindi kwenye kilele cha Siku ya Chakula Kimataifa Oktoba 16, 2025 na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa. 


Timu nyingine zilizoshiriki na viongozi wake kwenye mabano ni  namba 002 (Halfan Mnyeto), 007 (Mohamed Salim), 003 (Hamza Nguzo), 008 (Hussein Seif), 011 (Veso Kileo), 005 (Akida Koja), 001 (Kassim Abdi) na 006 (Jumaa Kibao).


Kaimu Mkurugenzi wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Nankondo Senzira, amesema mashindano hayo ni kilelezo cha ukweli kuwa uvuvi una mchango mkubwa katika ajira, lishe bora, kipato na fedha za kigeni.

Hivyo, amesema muhimu kuwepo ubunifu kama kufanyika kwa mashindano na kuwazawadia wavuvi ili kuonesha thamani na kuongeza tija katika shughuli zao.


Ametoa mfano kuwa mwaka 2024, uvuvi ulichangia asilimia 1.8 ya pato la taifa huku ikitoa ajira kwa Watanzania takribani milioni 6.


Mwakilishi Msaidizi wa FAO, Charles Tulahi, alisema mashindano hayo yanaendelea mpango wa kuzitafakari changamoto dhidi ya uzalishaji wa chakula ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, migogoro, gharama za maisha na kupungua kwa rasilimali kama ardhi, maji na bioanuai.


“Mashindano haya ya ngalawa siyo tu burudani, yana ujumbe kuhusu umuhimu wa Bahari na sekta ya uvuvi katika kuhakikisha usalama za chakula, lishe bora na ajira kwa jamii zetu,” alisema.


Alisema, yamefanyika kwenye Bahari ya Hindi iliyo hazina kubwa ya maliasili kwa samaki na viumbe wengine ambavyo ni chanzo cha protini, mafuta yenye afya na madini yanayosaidia ukuaji wa mwili na ubongo.


Risala ya washiriki wa shindano hilo ilieleza kuwa, wavuvi walitumia mwelekeo wa upepo, mawimbi na mbinu za jadi, na hivyo kuwawezesha kumaliza salama kwa kila mmoja wao.


Kwa mujibu wa risala hiyo, mashindano hayo yameonesha azma ya Serikali na wadau wake kuwatambua, kuwathamini na kuwashirikisha wavuvi wanaojinasibu kuwa mashujaa wa chakula na afya za watu nchini.


MWISHO

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »