TRA Dodoma Yawataka Wafanyabiashara Kulipa Kodi Kabla ya Septemba 30

September 23, 2025
Na. Yahya Saleh, Dodoma

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma Bw. Pendolake Elinisafi amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa kodi ya awamu ya tatu kwa wakati kabla ya tarehe 30.09.2025 ili kuepuka faini zisizo za lazima.

Akizungumza wakati wa zoezi la elimu ya kodi mlango kwa mlango linalofanyika mkoani Dodoma, Meneja huyo ameeleza kwamba, kodi zikilipwa mapema zitasaidia serikali kutekeleza mipango ya maendeleo kwa wakati.

"Nachukua fursa hii kutoa rai kwa walipakodi wa Mkoa wa Dodoma kulipa kodi ya awamu hii ya tatu kwa wakati ili serikali nayo iweze kutekeleza mipango ya maendeleo kama ilivyokusudia," alisema Bw. Elinisafi.

Aidha, amewaomba wafanyabiashara kutumia fursa ya zoezi hilo la elimu ya kodi mlango kwa mlango kwa ajili ya kutoa changamoto zao za kikodi zinazowakabili ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wao wafanyabiashara waliotembelewa katika zoezi hilo, wameipongeza TRA kwa kuja na kampeni hiyo huku wakiziomba Mamlaka nyingine za serikali kuiga mfano wa TRA ili kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo yao kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hizo.

Kampeni hiyo ya elimu ya kodi mlango kwa mlango imeanza tarehe 22 Septemba, 2025 mkoani Dodoma na itamalizika Oktoba mosi, 2025 ikiwa na lengo la kuwaelimisha walipakodi, kuwatambua walipakodi wapya na kuwasajili sambamba na kusikiliza maoni, ushauri na changamoto mbalimbali za kikodi zinazowakabili ili kuzitatua kwa haraka.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »