TANESCO YAIBUKA KINARA TATHIMINI YA UTENDAJI KAZI WA TAASISI ZA WIZARA YA NISHATI

September 29, 2025


📌Yawa mshindi wa kwanza kiutendaji na kuzawadiwa Kiasi cha shilingi Milioni Tano


📌utoaji huduma bora kwa wananchi ndani ya wakati na kuimarika kwa mawasiliano  ya haraka kwa wateja wake miongoni mwa vigezo vya ushindi 


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeibuka mshindi wa kwanza  katika tathmini ya utendaji kazi wa robo ya nne ya mwaka 2024/2025, baada ya kuongoza kati ya taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati. 


Ushindi huo umekuja baada ya tathmini ya utendaji kazi iliyofanywa na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini cha Wizara ya Nishati. 

Hayo yamejitokeza wakati wa kikao cha Tano cha Tathmini ya utendaji kazi wa Wizara ya Nishati  na Taasisi zake kwa robo nne ya mwaka 2024/2025 kilichofanyika  tarehe 26 Septemba 2025 jijini Dodoma  na kuongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba.


Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, ameipongeza sana TANESCO kwa jitihada zake za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na taarifa kwa wakati. Alisisitiza kuwa hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa utendaji kazi wa wizara na kuakisi dhamira ya Serikali ya kuboresha sekta ya nishati.


Aidha, imeelezwa kuwa mikoa ya TANESCO nayo imeendelea kufanya vizuri, ikiwemo Manyara, Kinondoni Kusini na Simiyu ambazo zimeibuka vinara katika tathmini ya mikoa. 


Hali hii inathibitisha kuwa TANESCO inaendelea kwa kasi na maboresho yenye tija katika kuimarisha utoaji wa huduma ya umeme kwa Watanzania wote.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »