REA YASAMBAZA MAJIKO NA MITUNGI YA GESI KILO 15 KWA JESHI LA MAGEREZA MKOANI SHINYANGA

September 24, 2025

 

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tarehe 24 Septemba, 2025 imesambaza kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza 221 mkoa wa Shinyanga majiko ya gesi ya sahani (2) na mitungi ya kilo 15 kwa ajili ya Maafisa na Watumishi wa Jeshi hilo huku wito ukitolewa wa kuwataka wawe mabalozi wa nishati safi kwa mkoa huo.

Katika hafla hiyo ya ugawaji wa majiko na mitungi ya gesi, Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Mhandisi, Ahmed Chinemba ametoa wito kwa Watumishi wa Jeshi hilo huku akieleza mkataba wa kusambaza teknolojia mbalimbali za nishati safi kati ya Wakala na Jeshi hilo, ulisainiwa mwezi Septemba, mwaka 2024 kwa gharama ya shilingi bilioni 35 kwa Magereza 129 Tanzania Bara.

Chinemba amesema Maafisa wa Magereza wanatakiwa kuwa mabalozi katika utumiaji wa teknolojia za nishati safi kama majiko ya gesi na kuongeza kuwa Wananchi wengi wa maeneo ya vijijini wanakata miti hovyo kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.

“Ninawapongeza Jeshi la Magereza kwani wamekuwa vinara wa matumizi ya nishati safi kwenye Magereza yote ukilinganisha na Taasisi nyengine sawa sawa na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu kuzitaka Taasisi zinazohudumia Watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi kama gesi; gesi vunde, mkaa na kuni mbadala”. Alisema Mhandisi, Chinemba.

Chinemba amesema katika utekelezaji wa Mradi huo, REA imechangia shilingi bilioni 26 na Jeshi la Magereza limetoa shilingi bilioni 8 ambapo ushirikiano huo umelenga katika maeneo kadhaa ikiwemo ujenzi wa miundombinu 126 ya bayogesi na majiko banifu 377; Ujenzi wa miundombinu 64 ya LPG na majiko banifu 256; Usambazaji wa mitungi ya gesi 15,126 ya kilo 15 pamoja na majiko ya gesi ya sahani mbili kwa watumishi wote wa Magereza; Usambazaji wa mkaa unaotokana na makaa ya mawe (Rafiki briquettes) tani 850 na majiko banifu 344 kwa kambi 129 za Magereza na maeneo mengineyo.

Naye, Mkuu wa Magereza mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Nobert Ntacho ameishukuru Serikali kupitia REA na kukiri kupokea mitungi ya gesi na majiko ya sahani mbili na kusema familia za Watumishi wa Jeshi hilo, wanakwenda kunufaika ambapo tayari wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya nishati safi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza wilaya ya Shinyanga; Kamishina Msaidizi, Martin Kunambi amesema Gereza linahudumia mahabusi 263 na kuongeza kuwa walishajenga miundombinu ya kupikia tangu Rais Samia Suluhu Hassan atoe maelekezo ya kuzitaka Taasisi zenye kuhudumia Watu zaidi ya 100 kuacha matumizi ya nishati zisizo safi na salama kama kuni na mkaa na kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi na salama

“Tunaipongeza na kuishukuru Serikali, leo tumepokea majiko na mitungi ya gesi ipatayo 221 sawa na idadi ya askari na Watumishi waliopo hapa mkoa wa Shinyanga” amesema Bwana Kunambi.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »