Na. Edmund Salaho - Tanga
Kamishna wa Uhifadhi TANAPA CPA Musa Nassoro Kuji ambaye pia ni mlezi wa HIFADHI SACCOS LTD ametoa wito kwa watumishi wote wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania kujiunga pamoja na kuanzisha SACCOS moja kwa watumishi wote wa TANAPA itakayoitwa TANAPA SACCOS LTD.
Kamishna Kuji ameyasema hayo leo Septemba 24, 2025 katika Mkutano Mkuu wa mwaka 2025 wa HIFADHI SACCOS unaofanyika Jijini Tanga.
"Ninafahamu kuwa kulikuwa na timu maalum ya uhamasishaji ambayo ilipita katika vituo vyote vya kazi kuhamasisha watumishi kufahamu faida za kuwa na SACCOS moja na kuwaomba watumishi wawe tayari kuunga mkono suala hilo muhimu. Mimi pia katika ziara zangu katika vituo vyote katika Shirika nimewasihi watumishi kukubali wazo la kuwa na SACCOS moja. Katika maeneo yote niliyopita, watumishi wamenihakikishia kuwa wazo hilo ni wazo jema na wapo tayari kuliunga mkono wakati ukifika".
Akitaja faida chache zitakazopatikana kwa kuwa na SACCOS moja, Kamishna Kuji alibainisha kuwa popote kwenye umoja pana nguvu ya mafanikio na hivyo mtaji wa Chama utaongezeka maradufu na kuifanya SACCOS hiyo iaminike na Serikali na taasisi nyingine za kifedha nchini.
Aidha, ameutaka Uongozi wa HIFADHI SACCOS kuendelea na uhamasishaji wa kupata wanachama zaidi ambao wataunda TANAPA SACCOS. Pia. Chama kuendelea kubuni mazao mapya na bora zaidi yatakayowanufaisha mwanachama pamoja na kuwekeza katika teknolojia ili kuwasaidia wanachama kufanya shughuli za kichama kidigitali.
Naye, Mwenyekiti wa Hifadhi SACCOS Philip Mwainyekule aliueleza Mkutano Mkuu wa 2025 kuwa Mchakato wa kuunda SACCOS moja ya Shirika zima umeendelea vizuri kwa msaada wa Sekretarieti iliyoundwa ambapo uliweza kutembelea Hifadhi zote ili kutoa elimu ya Ushirika kwa watumishi pamoja na kuandikisha wanachama waanzilishi wa TANAPA SACCOS na hadi sasa jumla ya watumishi 665 wameshajiandikisha kuwa wanachama wa TANAPA SACCOS.
Ushirika wa akiba na mikopo mahali pa kazi ni nyenzo muhimu katika kupata utatuzi wa mahitaji ya kifedha kwa gharama nafuu kwa watumishi ambapo wanaweza kupata rasilimali za kuendesha maisha yao.
EmoticonEmoticon