Dar es Salaam. Tarehe 8 Septemba 2025: Baada ya saa 72 za maboresho ya mfumo wa uendeshaji wa benki (Core Banking System), huduma za Benki ya CRDB sasa zimerejea zikiwa bora, zenye kasi kubwa zaidi kukidhi viwango vya kimataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema Benki iliweka juhudi kubwa kuhakikisha jambo hili linakmailika kwa wakati ili kurejesha huduma kwa wateja na wadau wake wengine katika majukwaa yote kama ilivyoahidi katika taarifa yake kwa umma iliyoitoa Jumatano tarehe 03 Septemba 2025.
“Benki ya CRDB ni taasisi ya kimataifa tukiwa tunatoa huduma nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huku tukikamilisha utaratibu wa kuingia Dubai. Huwezi kutoa huduma katika mataifa haya yote bila kuwa na mfumo imara utakaotunza taarifa za wateja na kufanikisha miamala kwa ufanisi mkubwa. Hii ni moja ya sababu iliyotufanya tuboreshe mfumo wetu mkuu wa uendeshaji. Ninafurahi kuwaeleza kwamba zoezi hili limekamilika kwa ufanisi mkubwa,” amesema Nsekela.
Nsekela amesema kilichokuwa kinafanyika ndani ya saa hizo 72 za kuhama kutoka mfumo wa zamani kwenda huu mpya, ni kuhamisha taarifa za wateja wote waliopo na kuruhusu usajili wa wateja wapya ndani na nje ya Tanzania ambako Benki ya CRDB inahudumia.
Kwa kutambua kwamba Benki ya CRDB inahudumia mamilioni ya wateja ambao walipata taarifa za maboresho haya kwa nyakati tofauti, lakini wote walionesha utulivu na kuiruhusu menejimenti itekeleze maboresho yaliyokusudiwa kwa utulivu mkubwa.
“Kwa ukubwa wa maboresho hayo yaliyohusisha kuhama kutoka kwenye mfumo wa zamani kwenda kwenye mfumo mpya, tulilazimika kusitisha huduma matawini na baadhi ya huduma mbadala (alternative channels) kutopatikana kwa muda. Nawashukuru sana wateja wetu kwa uvumilivu na ushirikiano waliotuonesha katika kipindi hiki na ninawaomba radhi kwa changamoto walizokutana nazo kwa muda ambao baadhi ya huduma zetu hazikupatikana,” amesema Nsekela.
Kutokana na kutoa huduma katika mataifa tofauti ambako kuna utofauti wa sheria, lugha na utamaduni, Nsekela amesema mfumo huu unawaruhusu wateja wa Benki ya CRDB kupata huduma kwa lugha waitakayo na sarafu waipendayo.
“Lugha rasmi kwa Tanzania ni Kiswahili na Kiingereza wakati Burundi wanatumia Kifaransa na Kirundi. Ukienda DRC wao wanazungumza Kifaransa na lugha zao nyingine wakati Dubai kuna Kiarabu na lugha nyingine za kimataifa. Huko kote, mteja atahudumiwa kwa lugha anayoitaka na atafanya miamala yake kwa sarafu aipendayo,” amesisitiza Nsekela.
Ili kuwatoa wasiwasi wateja wake hasa walioona mabadiliko kwenye salio na maeneo mengine ya huduma, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile amesema kulitokana na kuhama kutoka mfumo wa zamani na kuingia katika mfumo mpya ambao una usalama wa hali ya juu, wenye uwezo wa kutoa huduma mpya na bunifu za kidijitali na uliojengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
“Wote walioona tofauti kwenye salio na maeneo mengine, wajue kuwa hali hiyo ilitokana na kuhamisha taarifa kutoka mfumo wa zamani kwenda mfumo mpya. Wateja wetu wafahamu kwamba hatukuwa tunaboresha mfumo bali tulikuwa tunahama kabisa kuruhusu viwango vya mataifa mengine na taasisi za kimataifa tutakazokuwa tunashirikiana nazo,” amesema Mwile.

Maboresho haya yamefanyika ukiwa ni mwendelezo wa mapinduzi yanayofanywa na Benki ya CRDB katika kipindi hiki inaposherehekea miaka 30 tangu kuanzishwa kwake ikishiriki kwa kiasi kikubwa katika kukuza kipato cha mwananchi mmojammoja pamoja na kuimarisha uchumi wa taifa.
EmoticonEmoticon