KUMCHAGUA RAIS DKT SAMIA NI KUCHAGUA MAENDELEO -DKT.BITEKO

September 09, 2025



📌 Awahimiza wananchi wa Namonge kujitokeza kupiga kura Oktoba 29


📌  Asema shilingi bilioni 200 kukopeshwa kwa vijana


Mgombea wa Ubunge Jimbo la Bukombe, Ndugu Doto Mashaka Biteko amewaasa wananchi wa Kata ya Namonge, kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba kumpigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais kwa kuwa ndiye mwenye nia thabiti ya kuwaletea maendeleo.


Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 9, 2025 katika mkutano wake wa kunadi sera kwa wananchi wa Kata ya Namonge wilayani Bukombe mkoani Geita.

Amesema awali sekta zote katika kata ya hiyo zilikuwa zikisuasua kimaendeleo ikilinganishwa na maendeleo yaliyofikiwa sasa


“Kata hii haikuwa na barabara ya kutoka Uyovu - Namonge - Nyalamandula haikuwa na zahanati wala shule za kutosha hivyo ilikuwa na maendeleo duni” amesema Dkt. Biteko.



Amesema jitihada zilizofanywa na Serikali ya Rais Samia katika kuwaletea maendeleo wananchi hao ni kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati na kituo cha afya.


“  Nataka niwahakikishie mkinichagua tutaongeza wodi na zahanati, tunataka watu wa Namonge waishi kama Watanzania wa daraja la juu, Tutahakisha tunaongeza shule, kuna vijiji havikuwa na shule na tumejenga shule mpya. Tumekuja hapa kuomba kura ili tumchague Rais Samia kwa vile ni kumchagua yeye ni kuchagua maendeleo,” amesema Dkt. Biteko.

Ameelezea matarajio ya CCM ni kuifanya Kata ya Namonge iwe kituo cha kilimo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara na hospitali.


Pia, amesema CCM ikipata ridhaa ya kuongoza  katika miaka mitano ijayo Serikali itatoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwakopesha vijana ili wazitumie kwa kufanya biashara sambamba na kutoa mikopo kwa wanawake na watu wenyeulemavu.

“Namonge ina wapiga kura zaidi ya 30,000 hivyo nawaomba Oktoba 29 mwaka huu tujitokeze kwa wingi tukampigie  kura Rais Samia. Tunachotaka ni maendeleo na nataka kuwahakikishia Rais Samia anatupenda mno Bukombe na mwezi Oktoba atakuja hapa. Heshima  pekee tutakayompa Rais wetu ni kumpigia kura kwa wingi, msiniangushe,” amesisitiza Dkt. Biteko.


Akimnadi mgombea udiwani wa Namonge, Mlalu Bundala amesema ni mtu makini anayejua shida za wananchi na yuko tayari kuhakikisha Kata hiyo inapata maendeleo.


Naye, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Geita, Amani Msuwa amesema kuwa Rais Samia ametekeleza miradi mingi ya maendeleo mkoani humo hivyo Oktoba 29 wananchi wampigie kura pamoja na  mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.


Mgombea wa Udiwani  Kata ya Namonge, Mlalu Bundala amewashukuru wananchi wa Kata hiyo kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo.


Aidha, amesema katika Kata yake,  Rais Samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya km 61, mtandao wa maji Namonge wenye mita za ujazo 21, shule za msingi 7, shule za sekondari 3 pamoja na kituo cha afya.


Ameongeza kuwa Kata hiyo ina mtandao wa umeme katika vijiji vyote na jitihada za kufikisha umeme kwenye vitongoji zinaendelea.


Mwisho.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »